29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbasha amwaga machozi mahakamani

mbashaNa Veronica Romwald, Dar es Salaam
MWIMBAJI wa muziki wa injili, Emmanuel Mbasha, anayekabiliwa na kesi ya kumbaka mtoto wa miaka 17, jana alitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Ilala akibubujikwa machozi.
Hali hiyo ilimtokea mara baada ya shahidi wa pili wa kesi hiyo, aliyejulikana kwa jina la Suzan, kutoa ushahidi wake.
Kwa kuwa kesi hiyo inasikilizwa kwenye chemba (chumba maalumu ambacho waandishi na watu wasiohusika hawaruhusiwi kuingia) haikuweza kujulikana mara moja ni kitu gani kilichofanya mwimbaji huyo ambaye kwa sasa ameachana na mkewe, Flora Mbasha alie.
Mara baada ya kesi hiyo kuahirishwa na Mbasha kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo akiwa na wakili wake, Ngassa Ganja, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alisema shahidi huyo aliieleza mahakama jinsi binti anayedaiwa kubakwa alivyomsimulia namna alivyotendewa kitendo hicho.
Alisema shahidi huyo alitoa ushahidi wake mbele ya hakimu Flora Mjaya.
“Mnakumbuka ile siku ambayo shahidi namba moja (binti aliyebakwa) alivyoieleza mahakama kwamba walikwenda kwa dada yake kumtafuta Flora ndipo akabakwa na Mbasha? Basi huyu shahidi namba mbili (Suzy) ndiye yule dada yake,” alifafanua.
Katuga alisema shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alipata taarifa zote hizo baada ya binti anayedaiwa kubakwa kukimbilia nyumbani kwake na kumpa taarifa zote.
“Lakini kwa mujibu wa sheria (CPA) namba 186 kifungu kidogo cha tatu, inanizuia kueleza kwa kina yale ambayo shahidi huyo ameieleza mahakama,” alidai Katuga.
Kwa upande wake, wakili wa Mbasha, Ganja, aliliambia MTANZANIA kuwa licha ya shahidi huyo kueleza kwamba binti anayedaiwa kubakwa alipigwa na Mbasha, yeye shahidi hakumkagua ili kujiridhisha kama ni kweli alipigwa ama la.
“Ni kweli ameieleza mahakama ushahidi ambao Katuga amewaeleza, ila shahidi huyo hakumkagua (binti aliyebakwa) ili kujua kama ni kweli,” aliongeza.
Mbasha alifika mahakamani hapo mapema saa tatu asubuhi.
Hata hivyo kesi hiyo iliahirishwa kwa muda kutokana na wakili wake, Ganja kuchelewa kufika mahakamani hapo.
Ilipofika saa tano, kesi hiyo iliitwa tena na ushahidi huo kusikilizwa kwa takriban saa mbili, mbele ya hakimu Mjaya.
Katika kesi hiyo Mbasha ambaye ni mume wa mwimbaji maarufu wa muziki wa injili, Flora Mbasha, anadaiwa kumbaka shemeji yake mwenye umri wa miaka 17, kati ya Mei 23 na 25 mwaka jana eneo la Tabata ambako alikuwa akiishi naye.
Septemba 5 mwaka jana, binti huyo aliieleza mahakama kuwa alibakwa na shemeji yake huyo kwa awamu mbili tofauti kabla ya kufanikiwa kukimbia.
Kesi hiyo inasikilizwa mahakamani kwa siri kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles