27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

HII NDIO AZAM FC: MIAKA TISA KWENYE LIGI, MAKOCHA NANE

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


 

azam-fcTIMU ya soka ya Azam FC ilifunga mwaka 2016 kwa kuchukua maamuzi magumu ya kusitisha mikataba ya makocha wake kutoka Hispania, ambao wamedumu nao kwa muda wa takribani miezi sita.

Makocha waliofungashiwa virago ni Zeben Hernandez, msaidizi wake Yeray Romero, kocha wa makipa Jose Garcia, kocha wa viungo Pablo Borges na mtaalamu wa tiba za viungo, Sergio Perez.

Sababu kubwa ya Wahispania hao kutimuliwa ilidaiwa kuwa ni matokeo yasiyoridhisha waliyoyapata katika michezo 17 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Hernandez anaondoka Azam ikiwa ni miezi minne tangu alipochukua mikoba ya Muingereza Stewart Hall, ambaye aliamua kubwaga manyanga.

Kuvunjwa kwa mkataba wa Hernandez kunatimiza idadi ya makocha nane waliowahi kufanya kazi na Wanalambalamba hao katika kipindi cha miaka tisa tangu walipopanda daraja na kucheza Ligi Kuu.

Ikumbukwe Azam FC ilipanda daraja mwaka 2007 na imeshabadili makocha mara 11 (Hall ambaye ameinoa timu hiyo katika vipindi vitatu), hivyo Azam ina wastani wa kufukuza kocha kila mwaka.

Kitendo cha kubadilisha makocha mara kwa mara, huku wakiwa wametwaa taji moja tu la Ligi Kuu, Kombe la Kagame na Ngao ya Jamii inasababisha kuzua maswali mengi, kubwa mojawapo ni kweli tatizo ni makocha au kuna mengine yaliyojificha nyuma ya pazia?

SPOTIKIKI inakuletea orodha ya makocha waliopita katika timu hiyo na kile walichokifanya kuanzia walipopanda daraja.

 

Mohammed King (Zanzibar)

Nyota huyu wa zamani wa Small Simba, ndiye aliyeipandisha timu hiyo daraja, kutoka Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Ilala hadi kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008-2009.

Mara baada ya timu kupanda daraja, uongozi ulifanya mabadiliko ya benchi la ufundi kutokana na kanuni kuwabana na hivyo kumpa majukumu kocha aliyewahi kuinoa Simba, Neider dos Santos.

 

Neider dos Santos (Brazil)

Kocha huyo alitua Azam kwa mbwembwe, ambapo katika misimu yake ya awali aliifanikisha timu hiyo kumaliza nafasi ya nane ikikusanya pointi 26 baada ya kucheza mechi 22, ikiwa imeshinda saba na sare tano, ikipoteza michezo 10.

Hata hivyo, mabosi wa Azam walionekana kutoridhishwa na nafasi waliyofikia kwenye msimamo, uamuzi uliofuata ukawa ni kumfungashia virago na kumleta aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Itamar Amorim.

 

Itamar Amorin (Brazil)

Mbrazil huyo ndiye aliyechukua mikoba ya ndugu yake msimu wa 2009-2010 na kwa kipindi chake alifanya kazi nzuri ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu, nafasi tano tofauti na Dos Santos alivyomaliza msimu mmoja kabla yake.

Azam ya Itamar ilimaliza na pointi 33 kutokana na mechi 22, huku ikishinda nane na kupata sare tisa, ikipoteza tano tu, lakini licha ya kupandisha kiwango cha timu kocha huyo mkataba wake ulivunjwa na mikoba kukabidhiwa Hall, wakati lengo la uongozi likiwa ni kupata ubingwa wa Ligi Kuu.

 

Stewart Hall (England)

Angalau Muingereza huyu, aliweza kudumu kwa muda mrefu kidogo kwani, alitoka nayo mwaka 2010 hadi 2012, aliiwezesha Azam kuwa tishio kwa klabu za Simba na Yanga.

Katika vipindi vyake, Azam FC iliweza kutwaa taji moja tu la ligi na Kombe la Mapinduzi mwaka 2012, baada ya kuichapa Jamhuri ya Zanzibar mabao 3-1.

Msimu wake wa kwanza wa 2010/11 Azam ilishika nafasi ya tatu, lakini ikipata ushindi wa mechi 13 kati ya 22 ilizocheza, ikikusanya pointi nyingi hadi mwisho wa msimu (43) ambazo ni ongezeko la pointi 10 kutoka msimu uliopita.

Msimu uliofuata wa 2011/12, Hall aliiwezesha timu hiyo kuweka rekodi binafsi kwa kumaliza msimu ikiwa nafasi ya pili na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2013.

Katika mechi 26, iliweza kukusanya pointi 56 baada ya kushinda mechi 17. Kwenye mechi za kimataifa, Azam ilifika hadi raundi ya pili na kutolewa na FAR Rabat ya Morocco.

Mwisho wa ‘ndoa’ ya Hall na Azam ilikuwa ni baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga, kwenye fainali za Kombe la Kagame 2012, ambapo mabosi wa timu hiyo walisitisha mkataba wa Hall ambaye alitua Sofapaka ya Kenya.

 

Boris Bunjak (Serbia)

Bunjak ndiye aliyebeba mikoba ya Hall, lakini hakuchukua muda mrefu sana kabla ya kutimuliwa baada ya timu kuonekana kuyumba.

Bunjak aliiongoza Azam kwa muda wa miezi isiyozidi miwili kuanzia Agosti 2012 hadi Oktoba, kabla ya Azam kutoa kali ya mwaka kwa kuusitisha mkataba wake wa miaka miwili kisha wakamrejesha Hall kutoka Sofapaka.

Azam ilinufaika na kurejea kwa Hall, kwani ilirudi kwenye kiwango chake msimu wa 2012/13 walipomaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Licha ya kuipa taji la Mapinduzi, Azam ilimfungashia virago kocha huyo baada ya kuchemsha kwenye Kombe la Shirikisho, alipotolewa kwenye raundi ya awali na Ferroviario da Beira ya Msumbiji, lakini muda sio mrefu akapewa kibarua katika kituo cha kukuza soka la vijana cha Kidongo Chekundu kinachodhaminiwa na kampuni inayojihusisha na masuala ya umeme ya Symbion na klabu ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu England.

 

Joseph Omog-Cameroon

Kuondoka kwa Hall kulitoa nafasi kwa Mcameroon Omog kuinoa Azam, akiwa ametokea kuipa ubingwa AC Leopard ya Congo Brazzaville.

Omog alitua Azam huku ikiwa na moto, ikitoka kunyakua taji lao la kwanza la ligi.

Kocha huyo aliiongoza Azam kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014, lakini ikaondolewa mashindanoni katika raundi ya awali na El Merreikh ya Sudan.

Kutolewa huko ni kama kuliwachefua mabosi wa Azam, walioamua kuachana naye ikiwa ni baada ya kufanya vibaya pia katika Kombe la Mapinduzi, ambako waliondolewa na KCC ya Kenya.

Katika miaka yake miwili ndani ya Azam, Omog aliiongoza klabu hiyo katika mechi 55 zikiwamo 27 za ligi kuu, 19 ya michuano ya Kombe la Kagame, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Mapinduzi na michezo tisa ya kirafiki.

 

George Nsimbe (Uganda)

Mganda huyo maarufu kama ‘George Best’, alipewa mkataba wa muda kuiongoza Azam baada ya kutimuliwa kwa Omog, lakini akashindwa kuisaidia Azam kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, Azam ilimaliza katika nafasi ya pili kwa mara nyingine tena, kitu ambacho kiliwafanya mabosi wa Azam kufikiria suala la kumrudisha tena Hall kutoka katika kituo cha kidogo chekundu.

Ikiwa ni mara yake ya tatu, Hall kuinoa timu yao katika mechi za ligi na michuano ya kimataifa, kocha huyo aliisaidia Azam kutwaa taji lao la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame kwa kuifunga Gor Mahia kwenye fainali zilizochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, katika ligi msimu uliopita Azam ilishindwa kuonesha cheche licha ya kuwa chini ya jopo la wataalamu kutoka ulaya kwani, Yanga ilimaliza kwa kishindo mbele yao, huku Azam ikinusurika kupoteza nafasi ya pili.

Kabla ya kumalizika kwa ligi, huku Yanga wakiwa mabingwa, Hall alitangaza kuachana na Azam na kutoa nafasi ya kuletwa kwa kocha, Zeben Hernandez.

 

Zeben Hernandez (Hispania)

Kocha huyo aliyetua Azam akitokea klabu ya daraja la tatu ya CD Santa Ursula, alisaini mkataba wa miaka miwili na kuanza kibarua chake mwanzoni mwa ligi msimu huu.

Hernandez ameondoka Azam akiwa ameingoza kwenye mechi 17 za ligi na moja ya Ngao ya Jamii, ambapo amefanikiwa kushinda mechi nane, sare sita na kufungwa mara nne.

 

Idd Nassor Cheche

Amekabidhiwa mikoba ya Zeben kwa muda, kipindi ambacho mabosi wa Azam wanalisuka upya benchi la ufundi la timu hiyo.

Tayari Cheche ambaye ni kocha wa timu ya vijana wa Azam, ameisimamia timu hiyo katika mchezo mmoja wa ligi ambao wameshinda bao 1-0 dhidi Tanzania Prisons, lakini pia akipewa majukumu ya kuiongoza timu hiyo kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi katika muda huu wa kusaka kocha mwingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles