Na ASHA BANI
WAKATI Rais Dk. John Magufuli, akitangaza kuchukua hatua dhidi ya watendaji waliopandisha bei ya umeme nchini wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wametoa maoni yao juu ya suala hilo.
Akizungumza na MATANZANIA Dar es Salaam jana, Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema Shirika la Umeme (TANESCO) lisingeweza kukurupuka kupandisha bei ya umeme.
Alisema sababu kubwa ya kupandisha bei inatokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa, ili shirika hilo liweze kumudu gharama za uendeshaji.
Alisema licha ya shirika kushindwa kujiendesha lakini pia ni kutokana na mzigo mkubwa wa madeni unaolikabili shirika hilo.
Alisema baadhi ya madeni ni yale yanayochochewa na mikataba mibovu, hivyo shirika hilo linalazimika kutafuta fedha ya kulipia madeni yakiwemo ya IPTL na kwamba hakuna namna nyingine ya kufanya.
“Hapa kuna mambo matatu ambayo ili kulinusuru shirika la umeme yanatakiwa kufanyika ikiwa ni serikali kukubali kupandisha bei ya umeme au serikali kuchota fedha hazina ambazo zingeweza kufanyia mambo mengine ya maendeleo, kama vile kununua dawa, huduma za maji, miundombinu kuboresha na badala yake kupeleka Tanesco.
“…au vitu vyote vishindwe kufanyika na matokeo yake shirika lianguke kabisa kwa kushindwa kujiendesha,’’ alisema Kafulila.
Aliongeza kuwa Tanesco kwa sasa inamadeni makubwa yanayofikia Sh bilioni 600 inayotokana na mikataba mibovu, huku likikabiliwa na deni la Sh trilioni 320 zinazohitajika kuilipa Benki ya Standard Chartered .
Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), alisema Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo hana huruma ya kweli na Watanzania.
Alisema utaratibu wa kupandisha au kutopandisha umeme yanakuwa juu yao na kwamba waziri hana mamlaka ya kuingilia suala hilo.
Alisema amemsikia Waziri Muhongo akizungumza na redio moja kwamba tatizo lipo katika menejimenti ya Tanesco alisema ni uongo kwa kuwa tatizo hilo halikuanza jana wala leo, bali lilianza tangu 1995 mwishoni mwa utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Alli Hassan Mwinyi.
Alisema toka mwaka 1995 hakuna vyanzo vipya ya umeme vilivyojengwa zaidi ya vile vya Kidatu na Mtera jambo ambalo uzalishaji wa umeme unakuwa mdogo.
Hata hivyo alisema hasara nyingine zinatokana na Serikali kusimamia kidete kulipwa kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jambo ambalo litafilisi kabisa shirika hilo.
“Muhongo anajifanya yupo na watu, yupo na Watanzania lakini si kweli kwa nini alikubali kuilipa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL. Waziri huyu hashauriki, haambiliki, hivyo kama ataendelea kuwepo madarakani Watanzania wasubirie machungu,’’ alisema Kubenea.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarara Maharagande alisema Serikali iache kufanya kazi kwa mihemko na kisiasa.
Alisema hafikirii kama michakato yote iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) wenyewe walikuwa hawana taarifa hadi kufikia hatua ya kusimamisha bei mpya.
“Ni jambo zuri kuzuia upandishwaji huo wa umeme lakini sio jambo zuri kufanya mihemko ya kisiasa katika jambo la msingi kama hilo,’’ alisema.