24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA MUHONGO AFUATA NYAYO YA BULAYA  

Na BENJAMIN MASESE-MUSOMA


 

muhongoMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM), ameamua kufuata nyayo ya Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (CHADEMA) ya kuweka wazi matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo kwa wananchi.

Wiki iliyopita Mbunge wa Bunda,Bulaya aliamua kuchapisha vipeperushi vilivyoainisha matumizi  na mapato ya fedha za jimbo na kuvigawa kwa wananchi katika mikutano mbalimbali kitendo ambacho kilisifiwa na wakazi hao na kuondoa malalamiko yalikuwepo huenda fedha hizo zinatumika isivyo.

Naye Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Muhongo ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini, amejibu mapigo hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Tegeruka ambapo aliainisha fedha za awamu ya kwanza naya pili  na kuwaagiza wajumbe wa kamati ya mfuko huo kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ili kujiridhisha.

Akielezea fedha za awamu ya kwanza, alisema alipokea Sh 70,820,000 ambazo zilitumika kwa matumizi mbalimbali, ikiwamo Sh milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Murangi.

Profesa Muhongo, alisema Sh milioni 27.5 zilitumika kwa ajili ya kurekebisha nyumba na madarasa yaliyokuwa yameezuliwa na upepo kwa shule mbili za msingi, Sh  milioni 22.5 zilitumika kununulia mashine za umwagiliaji, mbegu za mbogamboga na matunda pamoja na dawa za kilimo na huku Sh  820,000 zilitengwa kwa ajili ya kuwezesha ufuatiliaji.

Alisema ni jukumu la kamati ya mfuko huo kuhakikisha fedha zimetumika kwa matumizi yaliyokubaliwa  kuagiza vikundi vyenye miradi ya kilimo ambavyo vilikabidhiwa vifaa na havijatumika mpaka sasa, wanyang’anywe na kuwakabidhi wengine  ili kuendeleza kilimo chenye tija.

“Tembeleeni hivi vikundi, mkikuta havijaanza kutumia vifaa tulivyowapatia mvinyanga’anye na vifaa hivyo vigawiwe kwenye vikundi vyenye nia ya dhati,” aliagiza Profesa Muhongo.

Akizungumzia awamu ya pili ya fedhaza mfuko wa jimbo, alisema alipokea Sh 38,479,000 ambazo alisema kamati husika kwa kushirikiana na wananchi pamoja na madiwani wamependekeza zitumike kwa ajili ya kuboresha kilimo.

Alisema Sh milioni 16 zitatumika kwa ajili ya kununulia mbegu za kisasa za mihogo za mkombozi kiasi cha vipando 532,000 ambazo zitagawiwa kwenye kata 21 kwa ajili ya vijiji 68 na Sh milioni 21.9 zitatumika kununulia mashine 21 za kukamulia alizeti.

Alisema hapo awali alisambaza mbegu za alizeti za majaribio kiasi cha kilo 4,000 ambazo zimeonesha mafanikio, aliongeza mbegu zilizoboreshwa kutoka Arusha kiasi cha kilo 5000 ambazo pia zilisambazwa.

Alisema ili kujiongezea kipato kutokana na kilimo cha alizeti, badala ya kuuza mbegu, wakulima hao wameamua kuuza  mafuta na ndiyo sababu ya kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya mashine hizo ambazo alizielezea kuwa ni za kuzungusha kwa mikono na hazihitaji mafuta wala umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles