25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JK: Kifo cha Komba ni pigo

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete amewaongoza mamia ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, wabunge, viongozi wa Serikali na wanasiasa wengine kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, huku akisema kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe ni pigo.
Alisema kifo cha Kapteni Komba kimeliondolea Taifa mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Rais Kikwete alisema: “Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba.
“Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye kiongozi wa kikundi cha sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi.
“Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake, ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa chama tawala. Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.”
Rais Kikwete aliwataka Watanzania wote kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.
Kutokana na msiba huo, aliwataka wananchi wa Jimbo la Mbinga Magharibi kutambua namna bora ya kumlilia mbunge wao aliyewapenda, ikiwamo kudumisha mema aliyoyafanya na kukamilisha kazi alizokusudia kuzifanya.
“Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.
“Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu. Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata,” alisema mkuu huyo wa nchi.

MAKINDA
Kabla ya shughuli ya kuaga mwili wa marehemu kuanza, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitumia fursa ya kutoa salamu za rambirambi kumwombea marehemu msamaha kwa umma kama kwa namna yoyote ile aliwakwaza.
Alisema kufariki dunia ghafla kwa Kapteni Komba ni sawa na moto wa kibatari, unavyoweza kuzimika wakati wowote.
“Kwa kuonyesha kwamba kifo hakina taarifa, na Mungu anavyotaka ndivyo inavyokuwa, ndiyo maana hata Jumamosi marehemu bado alikuwa akiendelea kuandika baadhi ya nyimbo zake.
“Ninaamini kama marehemu angepewa robo saa kabla ya kifo chake angesema maneno haya: ‘naomba msamaha kwa yeyote niliyemkosea’. Kwa sababu yeye ni binadamu, katika shughuli zake yawezekana kabisa kuna watu aliwakwaza, kwahiyo kama kuna mtu alimkosea, tumsamehe,” alisema Spika Makinda.
Alisema si vyema kwa baadhi ya watu kuendelea kumsema kwa mabaya marehemu.
“Baada ya kutokea kifo cha Kapteni Komba, baadhi ya watu wamekuwa wakitoa kauli za kumlaumu kwa maelezo kuwa wakati wa Bunge la Katiba, alizungumza maneno ambayo yaliwakwaza baadhi ya watu. Hili si sawa ndugu zangu,” alisema.

NYIMBO ZALIZA WATU
Wakati wa kuaga mwili wa marehemu Kapteni Komba, wasanii mbalimbali waliimba nyimbo maalumu ambazo ziligusa hisia za waombolezaji ambapo muda wote walikuwa wakibubujikwa machozi.
Mbali na wananchi wa kawaida, baadhi ya viongozi akiwamo Rais Kikwete na Spika Makinda, walishindwa kujizuia na kujikuta wakimwaga machozi.
Moja ya nyimbo zilizowagusa viongozi hao, ni ule ulioimbwa na wasanii wa dansi wakiongozwa na mkongwe King Kikii.
Kipande cha wimbo huo ambacho Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alighani, ndicho kilionekana kuwagusa wengi.
Baadhi ya maneno ya kipande hicho ni; ‘Komba akifika huko anakokwenda, amweleze Baba wa Taifa hali ya nchi ilivyo kwa sasa’.

KINANA
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema kishindo cha kifo cha mwanasiasa huyo ambaye pia ni msanii maarufu, kimezima sauti yake maarufu iliyojulikana na takribani Watanzania wote.
“Sauti zetu huzimwa na roho zikasimama kwa matakwa ya Mungu,” alisema Kinana.
Alisema huwezi kuzungumzia kukua na kuchanua kwa CCM bila kumtaja Komba aliyekuwa mkuu wa Idara ya Sanaa ya chama hicho, kwani nyimbo zake zilichangamsha wengi.
“Kwenye vita vya Kagera alikuwa anawahamasisha askari wetu, kwenye msiba wa Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliwafariji Watanzania, kifo chake ni pengo kubwa kwa CCM,” alisema Kinana.

NASSARI
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari (Chadema), aliyemwakilisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema pamoja na tofauti za kiitikadi, Kapteni Komba alimuheshimu bila kujali chama alichokuwa akitokea.
“Tumekuwa pamoja na Kapteni Komba katika kamati na wala hakuwahi kujali tofauti ya itikadi zetu za vyama, hasa linapokuja suala la taifa.
“Neno la faraja ambalo ningependa kuwaacha nalo ni lile lililo kwenye kitabu cha Zaburi linalosema; ‘Nitainua macho yangu nitazame milima, msaada wangu huu katika Bwana aliyezifanya mbingu na nchi’,” alisema.

SAID MTANDA ASIMULIA
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda, alisema Februari 24, mwaka huu alizungumza na Kapteni Komba kuhusu safari ya kamati waliyokuwa wanatarajia kusafiri kwenda nchini Ethiopia.
“Ilipofika Machi Mosi saa 10 nilipigiwa simu ya kuelezwa kwamba Komba ameaga dunia. Nilihuzunika kwa sababu alikuwa amana ya Serikali, chama, Bunge, jimbo lake la Mbinga Magharibi na wasanii aliokuwa akiwalea pamoja na Watanzania,” alisema.
Mtanda aliongeza kuwa ucheshi wa Kapteni Komba kwa wasanii na Watanzania, ulimfanya apachikwe jina la ‘Mlezi wa wana’.
Alisema uwezo wake na uzoefu ulichangia kubakishwa katika Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa muda wa miaka tisa, hali iliyomfanya kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo hadi kifo kilipomkuta.
Alimmwagia sifa Kapteni Komba kwa kusema alisaidia kuimarisha CCM, alitetea haki za wazee ili wapate matibabu bure na alipambana kutetea mswada wa habari.
Alisema pamoja na hivi sasa dunia kupambana katika mazingira, lakini Komba alipambana katika uhifadhi wa mazingira tangu mwaka 1984 kwa kuhamasisha upande wa Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

YUSUFU MAKAMBA
Akimzungumzia Komba, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba, alisema kuwa anaamini ameumizwa zaidi na msiba huo kuliko mtu mwingine.
“Nimefanya kazi na Kapteni Komba kwa miaka sita nikiwa Katibu Mkuu, nimefanya naye kazi sehemu mbalimbali ikiwamo kwenye uchaguzi mdogo ukiwamo wa Tarime,” alisema.
Alisema Komba alikuwa amana ambayo ililetwa na Mungu kwa ajili ya CCM, hivyo anaamini atakiletea chama mwimbaji mwingine mwenye uwezo kama wake.
“Naamini Mungu atatuletea mwimbaji mwingine ambaye atakuwa mzuri ingawa hatamfikia Komba, kwani siku zote jino la dhahabu haliwezi kuwa kama la fedha,” alisema Makamba.

PURUKUSHANI KUAGA MWILI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, umati wa wananchi ulifurika katika viwanja vya Karimjee kutaka kushuhudia safari ya mwisho ya Kapteni Komba, ambapo kila mmoja alitaka kutoa salamu zake za mwisho kwa kupita mbele ya jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu.
Hali hiyo iliwapa wakati mgumu waandaaji wa shughuli hiyo jambo lililofanya askari maalumu wa Bunge kuingilia kati na kupanga watu ili wote waweze kutoa heshima zao za mwisho.
Wananchi hao walipata fursa ya kuaga mwili huo baada ya Rais Kikwete, wabunge na viongozi wa chama na Serikali kutoa heshima zao za mwisho.
Kundi la mwisho kutoa heshima lilikuwa ni familia ya marehemu ambapo hisia na vilio vyao, vilifanya waombolezaji wengine kushindwa kujizuia.
Mara baada ya kuagwa, mwili huo ulisafirishwa kwa ndege kwenda mkoani Ruvuma ambako wananchi walipata fursa ya kuuaga katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamoja na Rais Kikwete na mkewe Salma, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali na wake zake, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na mkewe Sitti, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mkewe.
Wengine ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Spika Anne Makinda, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ali Abdallah Ali, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue.
Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Jaji Kiongozi, Shaban Ali Lila, Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi.
Pia walikuwapo Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha TLP na Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussen Katanga pamoja na mwanasheria wa kujitegemea Hashimu Rungwe.

Habari hii imeandikwa na Fredy Azzah, Shaban Matutu, Patricia Kimeremeta na Elizabeth Hombo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles