Na ATHUMANI MOHAMED
KATIKA maisha huwezi kupiga hatua ikiwa huna marafiki sahihi. Mtaji wa kwanza ni watu. Lakini lazima uwe makini sana na aina ya marafiki ulionao, maana wanaweza kukurudisha nyuma badala ya kuwa msaada kwako.
Tumeshajifunza somo la namna ya kuwajua na kuwaacha marafiki wasiofaa mwaka 2016 ili tukiingia mwaka mpya wa 2017 tuwe na marafiki wenye tija.
Wiki iliyopita niliahidi kuleta somo hili la marafiki unaopaswa kuingia nao mwaka 2017. Kama nilivyosema awali kwamba ni vizuri sana kuangalia aina ya marafiki ulionao.
Je, ni rafiki gani anafaa kuwa nawe kwa maendeleo yako? Yupi anafaa kuwa rafiki sahihi kwa maisha yako? Bila shaka utakuwa unao marafiki kadhaa, wengine unaamini ni wazuri na wapo ambao umeshagundua kuwa hawafai kuwa nawe tena.
Katika somo hili, tutaangalia marafiki ambao wanafaa kuwa nao katika kushauriana mambo mbalimbali ya maisha na ambao kwa hakika wanaweza kuwa chachu ya mafanikio yako.
Natambua wazi kuwa somo la maisha wengi huona kama ni gumu, lakini ndugu zangu nawaambia ukweli kwamba, ni vizuri sana kujifunza kila siku namna bora ya kuishi maisha safi yenye mafanikio.
Rafiki mwema wa kuwa naye 2017 ni yupi? Je, kati ya marafiki ulionao, ni wapi wa kuwaacha 2016 na wa kuingia nao mwaka 2017? Mada hii itakuwa msaada kwako.
KAULI ZAKE ZIKOJE?
Marafiki wa kweli siku zote huwa watu wa karibu wenye kupenda zaidi kusaidia. Jambo hilo huonekana hata kupitia kauli zao katika mazungumzo hata yale ya kawaida kabisa.
Kila mtu anahitaji kutiwa moyo kwa namna moja ama nyingine, katika mambo fulani fulani, sifa ambayo marafiki wa kweli huwa nayo.
Kwa mfano unaweza kuwa umepata ajali na ukampigia simu, rafiki asiye sahihi, atakimbilia kukuuliza maswali mengi. Mara oooh! Umeumia sana? Hujavunjika lakini? Unaendelea vizuri eeeh! Pole sana.
Mwenye upendo wa kweli, anayejua thamani ya urafiki wenu, haishii hapo. Atapenda kujua ulipo na kuja kukusaidia kwa namna anavyoweza.
Kauli bila kuchukua hatua, haina maana. Tathimini marafiki ulionao, kama yupo mwenye sifa hii, muweke pembeni.
Yule ambaye uliumwa, haraka akaja hospitalini na kukulisha chakula. Ambaye yupo nawe bega kwa bega kwenye matatizo yako, ndiye rafiki hasa wa kuingia naye mwaka 2017.
ANAYEKUSIKILIZA
Wakati fulani binadamu tunahitaji watu wanaofunga midomo na kutusikiliza. Nani asiyependa kusikilizwa? Hakuna. Sasa marafiki wa kweli wanaheshimu hilo na ikiwa upo kwenye mazungumzo naye, atafunga kinywa chake na kukusikiliza, mradi tu nawe huwa unamfanyia hivyo wakati fulani mnapokuwa kwenye mijadala.
Wapo makini kwenye mazungumzo na hukutazama machoni wakati ukiongea. Mara kadhaa humuona akitafakari kidogo unayosema. Muhimu kumbuka unachosema kwake, kisha baadaye mwulize maswali kuhusiana na kile ulichomwambia.
Angalia, je, alikuwa makini kukusikiliza? Anakupa ushauri mzuri? Ukiona hakuwa makini, maana yake, matatizo / mambo yako hayana umuhimu sana kwake. Kumbuka  mtu huyo huwa upo makini na mambo yake na huwa unamsaidia sana.
Wakati fulani unaongea naye, yeye yupo busy na simu, akipiga soga kwenye mitandao ya kijamii, ujue wazi hapo hakuna rafiki. Huu siyo wakati wa kupoteza muda kwa marafiki wasio na maana. Angalia ambaye ‘atakupa’ kama wewe ‘unavyompa!’.
Ikiwa kila siku, wewe ndiye mwenye kuwa makini na matatizo yako, lakini yako anaendelea na u-busy wake, huna sababu ya kuendelea kupoteza muda wako.
Unapaswa kuchukua hatua tu. Tutaendelea kuona sifa zaidi wiki ijayo.