Na Mwandishi Wetu-Lindi
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.
“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema wanafunzi wanaenda shule za msingi, kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Lindi, baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo Ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Waziri Mkuu aliwasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.
Alisema Serikali ya awamu ya tano, imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto sasa iweje watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari. “Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” amesema.
Aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi, lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili watachelewa.
“Kama tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri tutapata vijana wengi watakaohitimu kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.
“Tafuteni moja kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” amesema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema atafuatilia ili abaini ni kwa nini taasisi ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi mazao kwenye maghala hayo.
Alisema atapitia sheria ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama inaruhusu tozo hizo na kuangalia sheria gani inawaruhusu kutoza kodi. Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali inatoza tozo kwenye maghala ambayo yamejengwa na wananchi.
Akitoa mfano kuhusu ghala la Liwale, Waziri Mkuu alisema: “Kuna viagency (wakala) vimeanzishwa kazi yao ni kutoza mapato tu. Inakuwaje kunakuwa na taasisi imekaa tu na kuanza kutoza tozo kwa wananchi wanaotumia facility za Serikali. Sheria ya kutoza tozo imetokana na nini na hizo zinakwenda kwa nani, je Serikali imeanza kufanya biashara?,” alihoji.