28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

AUAWA AKIGOMBEA SODA

Na JANETH MUSHI – ARUSHA


charles-mkumboJESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha, Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo.

Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Morombo na kwamba aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.

“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally.

“Siku ya tukio, marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.

“Wakiwa ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.

“Kwa hiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani.

“Baada ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.

Wakati huo huo, RENATHA KIPAKA ANARIPOTI KUTOKA BUKOBA kuwa watu wanne mkoani Kagera wamefariki dunia katika matukio tofauti wakati wa Sikukuu ya Krismasi.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba.

Kamanda Ollomi aliyataja majina ya marehemu hao kuwa ni Dodo Jastine (30), mkazi wa Chanika, Kata ya Kanoni, wilayani Karagwe, ambaye alikutwa amefariki katika shamba la miti, mali ya Faustine Bwire akiwa amejeruhiwa sehemu za kichwa.

Mwingine ni mkazi wa Kanuguru, Tarafa ya Nyarumbugu, wilayani Biharamulo, aliyefahamika kwa jina moja la Suzana (42), ambaye aliuawa na mumewe kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

Mbali na hao, Kamanda Mkumbo alisema Kigozi Saimon (66), Mkazi wa Ntumagu, wilayani Biharamlo, alikutwa akiwa amefariki katika Barabara ya Nyakanazi na Mwalimu wa Shule ya Msingi Ombwea, Kata ya Kabirizi, Halmashauri ya Bukoba, Isiraeli Rugarabamu (52), alikutwa amejinyonga hadi kufa nyumbani kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles