27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

LWANDAMINA ATULIZA MASHABIKI YANGA

KOCHA mkuu wa Yanga, George  Lwandamina.
KOCHA mkuu wa Yanga, George Lwandamina.

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa Yanga, George  Lwandamina, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuahidi kuwa klabu hiyo itatetea ubingwa msimu huu licha ya kuachwa nyuma kwa tofauti ya pointi nne na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu kwa misimu miwili mfululizo, wanashika nafasi ya pili katika msimamo baada ya kufikisha pointi 37, huku vinara Simba wakishika usukani kwa kujikusanyia pointi 41.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Lwandamina alisema hawezi kuwaangusha wapenzi na mashabiki wa Yanga kwa kuwa anafahamu wanahitaji kutetea ubingwa wao msimu huu.

“Nitajitahidi kutumia uwezo wangu kuhakikisha ubingwa wa ligi kuu msimu huu unabaki Yanga kama mashabiki wanavyotarajia,” alisema Lwandamina.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Zambia alisema kuwa ili timu hiyo iweze kupata mafanikio ya kutetea ubingwa ni lazima wachezaji wajitahidi kucheza kwa bidii, kuongeza ushirikiano uwanjani na kujenga nidhamu ya juu nje na ndani ya uwanja.

Lwandamina alisema kabla ya kujiunga na Yanga alikuwa akiifuatilia kwa makini na sasa anaifundisha, hivyo mashabiki watulie matokeo ya kazi anayofanya yatajieleza kwao.

Mbali na kupambana kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, Yanga inakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo imepangwa kuanza hatua ya awali dhidi ya Ngaya de Mbe kutoka Visiwa vya Comoro.

Yanga itaanza kutupa karata yake ya kwanza kwa kucheza ugenini kati ya Februari 10-12 na mchezo wa marudiano utapigwa kati ya Februari 17-19 mwakani na endapo itashinda itakutana na mshindi kati ya Zanaco ya Zambia na APR ya Rwanda.

Kwa mara ya mwisho Yanga iliondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Al Ahly ya Misri na kuingia moja kwa moja kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ambapo ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Wakati huo kikosi cha Yanga kilikuwa chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm, ambaye sasa amepewa majukumu ya kuwa Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi.

Kocha Lwandamina aliyeipatia mafanikio makubwa kimataifa klabu ya Zesco United ya Zambia aliyokuwa akiifundisha kabla ya Yanga, ataiongoza timu hiyo kwa mara kwanza itakapovaana na Ngaya de Mbe ya Comoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles