29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Migiro ataka albino wasajiliwe

migiroNA EVANS MAGEGE
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, ameiagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kuwasajili watu wote wenye ulemavu wa ngozi nchini (albino), ili kurahisisha jitihada za serikali za kuwalinda.
Dk. Migiro alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizindua mkakati wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa wanafunzi wa shule za msingi Wilaya ya Kinondoni kwa kueleza kuwa matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamelitia doa Taifa katika uso wa kimataifa.
“Matukio haya yanaichafua nchi, ni ya aibu sana kwenye uso wa kimataifa, tunaonekana ni watu wa ajabu, hivyo kwa upande wetu kama serikali lazima tuwe na mkakati maalumu wa kuwatambua albino mahali wanakoishi ili vyombo vya dola vipate uhakika wa kuwaimarishia ulinzi zaidi.
“Katika matukio haya kuna changamoto nyingi, hasa familia zinahusishwa na mauaji ya albino, lakini kwa upande wetu serikali kwa kushirikana na jamii tuna wajibu wa kuwalinda albino kwa sababu ni binadamu wenye haki ya kuishi kama sisi,” alisema Dk. Migiro.
Awali Dk. Migiro aliupongeza mkakati wa RITA wa kusajili watoto walio kati ya umri wa miaka sita hadi 18 kuwa mpango huo utaisaidia serikali kupanua huduma za kijamii.
“Mnatakiwa kufahamu kuwa mfumo wa usajili wa vizazi, ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu za matukio muhimu ya binadamu ni mfumo muhimu na wa msingi katika shughuli za kiutawala na upangaji wa mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii kwa makundi yote,” alisema.
Alisema maisha ya mwanadamu yanaanzia pale anapozaliwa, hivyo tukio la uzazi maana yake ni ongezeko la idadi ya watu katika jamii na Taifa na serikali kwa upande wake inaongeza wajibu wa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa RITA, Phillip Saliboko, aliahidi kulifanyika kazi agizo la Dk. Migiro kwa kueleza ofisi yake itaanza utekelezaji wa usajili wa watu wenye ulemavu wa ngozi haraka.
“Hii ni changamoto, lakini ni lazima tukutane haraka kwa ajili ya ufumbuzi wake. Mauaji ya albino yanatugusa sote, nasi kama wakala lazima tuwasajili ili kuisaidia serikali kuwalinda,” alisema Saliboko.
Awali Saliboko alisema mkakati wa usajili wa watoto uliozinduliwa katika Wilaya ya Kinondoni, umelenga kuandikisha wanafunzi wa shule zote za msingi katika wilaya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles