25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRA KUSIMAMIA MAPATO YOTE YA SERIKALI  

NA KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


Ofisa Kodi Mkuu Sydney Mkamba
Ofisa Kodi Mkuu Sydney Mkamba

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepewa jukumu na Serikali la kuhakikisha inakusanya kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Sheria ya TRA sura ya 339 ya sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mabadiliko katika sheria ya fedha ya mwaka 2016 Julai mosi, TRA itapaswa kusimamia mapato yasiyotokana na kodi lakini itatekeleza hilo pale tangazo la Serikali litakapotolewa.

Lakini pia sheria ya kodi ya mapato ya 2004 inaelekeza utozaji wa kodi katika vianzio vya mapato ya biashara, ajira na uwekezaji.

Katika sheria hiyo kuna sheria 49 ambazo iwapo Serikali itatoa maelekezo kwa TRA basi mamlaka hiyo italazimika kuzisimamia.

Kwa upande wa sheria ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka 1995 yenyewe huelekeza uanzishwaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.

Pamoja na jukumu hilo lakini pia mamlaka hiyo imejiwekea mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha kufanikisha jukumu la Serikali la kukusanya kodi.

Miongoni mwa mikakati hiyo iliyojiwekea ni kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kodi kwa wafanyabiashara wa ndani na wa nje, taasisi za Serikali, binafsi na dini, shule za sekondari ambako wameanzisha klabu za kodi ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa makontena kwa kuyapiga picha yote badala ya moja kama ilivyokuwa awali.

Mikakati mingine ni kutowavumilia wafanyabiashara wote watakaokwepa kulipa kodi kwa makusudi ikiwa ni pamoja na kupeleka maofisa wake katika Chuo cha Polisi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kupata mafunzo ya kiaskari pamoja na mbinu zote za upelelezi na uchunguzi.

Kupelekwa kwa maofisa katika chuo cha mafunzo ya polisi ni mkakati ambao umewekwa kwa lengo la kuweza kuwaongezea mbinu za utendaji kazi maofisa wa TRA hasa wakati wa kufanya doria za kukamata magari yaliyokwepa kodi ikiwa ni pamoja na bidhaa haramu na za magendo zinazopitishwa kwenye mipaka isiyo rasmi, bandarini pamoja na kwenye bandari bubu.

Nchi nyingi zilizoendelea duniani ni kutokana na kodi mbalimbali za wananchi hivyo kila mtu anayestahili kulipa kodi anatakiwa kutekeleza jukumu hilo ili kuiwezesha nchi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii ikiwa ni pamoja na uchumi kukua.

Ili kuiwezesha Serikali kufanikisha malengo yake hasa ya Serikali ya uchumi wa  viwanda, watu wote wanaostahili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria wanatakiwa kuwa waaminifu na wazalendo kwa nchi yao kwa kuhakikisha wanalipa kodi.

Pia kwa mujibu wa sheria kuna baadhi ya taasisi ambazo hupewa msamaha wa kodi pindi wanapoingiza bidhaa au magari nchini kwa matumizi kulingana na kazi zao.

Lakini kama taasisi hiyo baadaye ikiamua kuliuza gari hilo kwa mtu asiye na msamaha bila kutoa taarifa kwa mamlaka atakuwa amechangia kuikosesha Serikali mapato yake.

Mbali na taasisi pia hata watu wanaotoka nchi jirani ambao huomba vibali kutumia magari yao kwa muda watakaokuwepo nchini lakini baadaye akiamua kuliuza bila mamlaka kuwa na taarifa pia atakuwa amechangia kuikosesha Serikali mapato.

Pamoja na maofisa wa TRA waliopitia mafunzo ya polisi lakini mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wanaziba mianya yote ya ukwepaji wa kodi ikiwa ni pamoja na kuzitaifisha bidhaa zote za magendo pindi wanapozikamata.

Ofisa Kodi Mkuu wa TRA, Sydney Mkamba, anasema ukamataji wa magari au magendo ni sehemu ya utendaji kazi wa TRA iliyojiwekea na kwamba lengo ni kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kwa hiyari.

Anasema kila gari hulipiwa kodi kulingana na aina pamoja na thamani yake, hivyo kama mtu amelinunua kutoka katika taasisi yenye msamaha wa kodi basi atapigiwa hesabu kulingana na uchakavu wa gari hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles