Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
NAHODHA wa Yanga, Haruna Niyonzima, amewataka wachezaji wa timu hiyo kushirikiana uwanjani ili kuuzoea kwa haraka mfumo mpya unaotumiwa na kocha Mzambia, George Lwandamina, vinginevyo wanaweza kushindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Yanga ilifanya mabadiliko ya kiufundi baada ya kumalizika mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumpa majukumu ya kuwa Mkurugenzi wa Ufundi aliyekuwa kocha mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm, huku Lwandamina akirithi mikoba yake.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Niyonzima alisema athari za mabadiliko ya mfumo ndani ya timu hiyo zinaweza kujitokeza katika mzunguko wa pili wa ligi, unaotarajia kuanza kutimua vumbi Jumamosi hii.
“Kocha wa sasa anatumia mfumo tofauti na ule tuliofundishwa awali, hivyo kama tunataka kutetea ubingwa ni lazima wachezaji tuungane na kukubali mabadiliko baada ya ujio wa Lwandamina.
Aidha kiungo huyo wa kimataifa kutoka Rwanda, alisema kipigo cha mabao 2-0 walichopata Jumamosi iliyopita katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya JKU ya Zanzibar kilitokana na mabadiliko ya mfumo wa uchezaji.
“Wapenzi na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuwa tayari kwa matokeo yoyote, kwani sasa mambo yamebadilika ndani ya kikosi,” alisema.
Alisema anaamini matokeo ya kufungwa kwenye soka ni jambo la kawaida, hivyo hawezi kushangaa ikiwa timu hiyo itapoteza mchezo katika mzunguko wa pili kutokana na mabadiliko yaliyopo kwa sasa.
Kikosi cha Yanga kinatarajia kuanza duru ya pili kwa kuvaana na maafande wa JKT Ruvu Jumamosi hii katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salam.