Na AMON MTEGA, SONGEA
JAMII imeshauriwa kutambua uchangiaji wa damu kwenye hospitali ni suala la lazima katika kuwasaidia wagonjwa wanapokwenda kupata huduma ya matibabu ya kuongezewa damu.
Wito huo umetolewa juzi na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Songea Revival (TAG), Severin Fussi, wakati alipokwenda kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya St. Joseph Peramiho.
Mchungaji Fussi ambaye aliongozana na waumini wa kanisa hilo kuchangia damu, alisema kila mwanajamii ajipime na kufanya uamuzi wa kuchangia damu kwa ajili ya ndugu, jamaa na marafiki.
“Baadhi ya watu bado wana fikra potofu kuwa kazi ya kupata damu ya kumtibia mgonjwa ni ya madaktari, hii si sahihi, ni suala la wanajamii nzima kutambua umuhimu huo wa kuchangia damu.
Mbali na damu, Mchungaji huyo alitoa msaada wa shuka 24 zenye thamani ya Sh 500,000 kwa wagonjwa.
Akishukuru msaada huo, Katibu wa hospitali hiyo, Mwajabu Mshana, alizitaka taasisi nyingine na watu binafsi kuunga mkono juhudi za mchungaji huyo.