26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

CHANGAMOTO ZA BARABARA INAYOKATIZA HIFADHINI MIKUMI

mikumi

Na EDITHA KARLO, MIKUMI

HIFADHI ya Taifa ya Mikumi, wilayani  Mikumi mkoani Morogoro, ni miongoni mwa hifadhi 16 zilizopo nchini.

Hifadhi  hiyo ina vivutio vingi na rasilimali muhimu kwa Taifa.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Donat Mnyagatwa, katika  mahojiano mahsusi anamwambia mwandishi wa makala hii kuwa pamoja na hifadhi hiyo kuwa na rasilimali nyingi na vivutio vingi, lakini pia ina changamoto nyingi za kutengeneza.

Mnyagatwa anazitaja changamoto zilipo hifadhini hapo kuwa ni ya kugongwa wanyama, hali inayosababishwa na uwepo wa barabara ya lami inayotoka Dar es Salaam na kukatiza ndani ya hifadhi hiyo ikielekea mikoa ya nyanda za juu kusini na Zambia.

“Wazo la kuwepo kwa barabara hii kupita katika hifadhi ni zuri, lakini kwasasa limekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wanyama, kwani wanyama wamekuwa wakigongwa na madereva wazembe kwa bahati mbaya au makusudi kwa magari mara kwa mara na kufa, hali itakayopelekea wanyama kupungua siku hadi siku hifadhini hapo,” alisema.

“Wastani wa mnyama mmoja anagongwa na gari na kufa na kwa mwezi wastani wa wanyama 29 wanapoteza maisha, hivyo ni vyema Serikali kuangalia  suala hilo kwa kina ili barabara hiyo inayopita ndani ya hifadhi  ibadilishwe  na ipitishwe njia ya Melela-Kilosa-Mikumi ili kuwanusuru wanyama na vifo visivyo vya lazima, ” alisema  Mnyagatwa

Alizitaja takwimu za ujumla ndani ya  miaka mitano zinaonyesha kuwa wanyama 956 waligongwa katika barabara hiyo, wakiwamo simba, chui, tembo, twiga na ndege na jamii ya mijusi.

Kati ya Januari na Februari mwaka huu, jumla ya wanyama 52 wamegongwa ndani ya hifadhi hiyo.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Tanapa ina mpango mkakati wa kufunga kamera maalumu zitakazowezesha kuwabaini madereva wanaogonga wanyama hifadhini ili wachukuliwe hatua za kisheria. Wataalamu wengine wanasema matumizi ya ‘drones patrols’ yangewezesha zoezi hilo.

Alisema changamoto nyingine inayosababishwa na uwepo wa barabara hiyo katika hifadhi ni baadhi ya mabaki ya chakula na uchafu unaotupwa na abiria wanaopita ndani ya hifadhi hiyo na magari na kusababisha baadhi ya wanyama kuacha kula chakula cha asili na kukimbilia barabarani kula vyakula vilivyotupwa na abiria.

“Wasafiri wanaotumia barabara inayokatiza hifadhini wamekuwa na tabia ya kutupa mabaki ya chakula, mifuko ya nailoni na hata chupa za maji ambapo baadaye wanyama hula na kupata madhara, kwani mnyama akila mfuko wa nailoni mfumo wake wa chakula hushindwa kufanya kazi vizuri  matokeo yake hufa,” aliongeza Mhifadhi.

Alisema pia baadhi ya takataka zinazotupwa, ikiwemo mifuko ya plastiki, chupa za maji n.k huchukua muda mrefu kuharibika na utupaji taka huo husababisha madhara ya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa watu, wanyama na mimea sambamba na uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha mazingira ya uoto wa asili ndani ya hifadhi.

Aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri wanaotumia barabara hiyo kujenga tabia ya kuweka vifaa vya kuhifadhia takataka katika vyombo vyao vya usafiri.

Changamoto nyingine katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi watu kufanya utalii wa bure wanapopita katika barabara hiyo na kusababisha Taifa kukosa mapato.

“Kipande cha barabara kinachopita hifadhini kina kilomita 50 ambapo watu hutumia muda wa takribani saa nzima kupita hifadhini na kuweza kuwaona wanyama karibu wote na hivyo kutokuona umuhimu wa kuingia hifadhini kulipia, hivyo kuikosesha hifadhi mapato na Serikali pia,” alisema.

Mnyagatwa alisema pamoja na uwepo wa vibao vya kuzuia mwendo kasi kwa madereva ambavyo ni mwendo wa kilomita 50 kwa saa, lakini kuna madereva wasiowaadilifu  hukimbiza magari kasi hifadhini na hivyo kuwagonga wanyama na kufa.

Alisema uwepo wa barabara hiyo ya lami hifadhini humo pia imechangia vitendo vya ujangili, hasa nyakati za usiku.

Usiku baadhi ya madereva wasiowaaminifu husimamisha magari yao katikati ya hifadhi na kujifanya wameharibikiwa na kufanya ujangili kwa urahisi na kuondoka kwa urahisi sababu barabara ni nzuri,” aliongeza.

Ameshindwa kuelezea kwa nini wasikaguliwe kwenye mageti yaliyopo na kuwabaini majangili hao.

Hata hivyo, Mnyagatwa anasema Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linatoa elimu kwa wasafiri kwa kupanda ndani ya mabasi ili kuwaelimisha abiria jinsi ya utunzaji wa mazingira na kuhifadhi takataka.

Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo mkuu, utupaji wa takataka ndani ya hifadhi hiyo unaharibu ikolojia ya wanyama, kwakuwa wanyama hao badala ya kula vyakula vya asili vinavyopatikana hifadhini humo, wao hukimbilia barabarani na kula vyakula visivyo vya asili vilivyotupwa na wasafiri.

Anasema ni vyema suala la uchafuzi wa mazingira pamoja na kudhibiti wanyama kugongwa katika Hifadhi ya Mikumi vikapewa umuhimu unaostahili.

Serikali imeshauriwa kutenga fedha za ujenzi wa barabara Melela-Kilosa-Mikumi yenye urefu wa kilomita 141.78 ili kupunguza idadi ya magari yanayopita ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema pamoja na changamoto zikizopo katika hifadhi hiyo, lakini Tanapa imeweka mipango mizuri ya kuendeleza hifadhi hiyo ya Taifa ya Mikumi na  kubainisha maeneo mapya yenye vivutio vya utalii na kutengeneza barabara na vivuko zaidi ili watalii waweze kufika kwenye vivutio kwa urahisi.

Anataja mikakati mingine kuwa ni kutengeneza barabara ya kuunganisha utalii wa Hifadhi ya Mikumi na pori la Selous, lililoko kusini  mwa  Reli ya Tazara, ili watalii wawepo hifadhini kwa siku nyingi na kuongeza mapato ya hifadhi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Alisema pia Tanapa imejenga nyumba kwa ajili ya watalii wa ndani na wa nje ya nchi na bei ya malazi inategemea na uwezo wa mtu, alisema pia malengo ya hifadhi hiyo ni pamoja na kujenga hosteli mpya kubwa na za kisasa ili kukidhi mahitaji ya wageni na kuongeza pato kutokana na malazi.

Naye Muikolojia mwandamizi anayesimamia kitengo cha uhifadhi ndani ya Hifadhi ya Mikumi, Crispin Mwinuka, anasema mtalii anapofanya shughuli zake za utalii ndani ya Hifadhi ya Mikumi anaweza kufanya utalii kwa miguu kwa kusindikizwa na kiongozi wa watalii na askari wa kulinda usalama ili asidhuriwe na wanyama wakali.

Mwinuka anasema mtalii anayefanya utalii ndani ya Hifadhi ya Mikumi anaweza kuona wanyama ambao ni vivutio kuwa chui, simba, mbwamwitu, tembo, twiga, nyati, kongoni, pofu, nguruwe pori pamoja na wanyama wengine wengi.

Anasema pia mtalii anaweza kuona mamba, viboko,   nyumbu, swala, nyani, ngedere, mbega, fisi, pundamilia, na aina mbalimbali za ndege wapatao 360, nyoka na wadudu.

Anasema hali ya mapito kwa wanyama waliopo katika hifadhi hiyo yanaonesha kuwa awali yalikuwa ni mapito ya asili ya wanyama yakiunganisha hifadhi za Mikumi eneo la Wami-mbiki, kusini mwa Mikumi na pori la akiba la Selous.

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Kijiji cha Doma, kilichokaribu na hifadhi yaTaifa ya Mikumi, wamesema wamekuwa wakitoa ushirikiano wa mara kwa mara kwa maofisa wa Tanapa kwa kuhakikisha hifadhi hiyo inakuwa safi na kupinga masuala ya ujangili.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0752202783 au email [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles