Na Ibrahim Yassin,Nkasi
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, imeipongeza Serikali kwa utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Nkasi,Desderius Mipata baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya, Said Mtanda ambaye alisema ilani hiyo inatekelezwa kwa vitendo.
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa yanaonekana kwa macho ni pamoja na kuendelea na kazi ya kuwabana watumishi wasiokuwa waaminifu.
Alisema suala la upatikanaji wa pembejeo,ukamilishaji wa miradi kadhaa ya maji ya mamilioni ambayo imegharimu mamilioni ya fedha ilisimama, lakini sasa inaendelea,ujenzi wa zahanati,vituo vya afya na upatikanaji wa dawa.
Alisema wamekuwa wakihamasisha watu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),utekelezaji wa utengenezaji wa madawati,ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu.
Alisema katika utekelezaji wa miradi mingi kama ambavyo wameelekezwa na ilani ya chama kuna baadhi imekwenda vizuri, lakini mingine ilikuwa na changamoto kadhaa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Zeno Mwanakulya aliwataka watendaji wa Serikali kukubali mabadiliko ya utendaji chini ya falsafa ya ‘’hapa kazi tu,’’ huku akimsihi mkurugenzi kuendelea kuwachukulia hatua watendaji ambao si waadilifu.
Mbunge wa Nkasi Kasikazini, Ally Kessy (CCM), alisema watahakikisha watumishi wasiowaadilifu wanachukuliwa hatua papo hapo.