NA EVANS MAGEGE,
TUHUMA za rushwa ambazo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alimtuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, sasa zimeifumba mdomo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mazingira ya Takukuru kufumbia mdomo tuhuma hizo yanatokana na msimamo mpya wa taasisi hiyo wa kukataa kuzungumza lolote juu ya mwenendo wa uchunguzi wa tuhuma hizo.
Awali, siku chache baada ya Makonda kumtuhumu Kamishna Sirro, Takukuru iliweka bayana kwamba inaanza mara moja uchunguzi wa tuhuma hizo.
MTANZANIA Jumapili lilitaka kufahamu mwenendo wa uchunguzi wa tuhuma hizo ambapo lilizungumza juzi kwa njia ya simu na Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba ambaye alikataa kulizungumzia sakata hilo.
Katika maelezo yake, Misalaba alisema Takukuru inafanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kisheria hivyo inaona si vyema kulizungumzia kwa kuhofia mvurugano wa kitaasisi.
“Unajua suala hilo kama ulikuwa unaangalia au kusikiliza kwenye vyombo vya habari na minong’ono mitaani utabaini kuna mambo mengi sana yaliyozungumzwa. Kutokana na hali hiyo, napenda nikufahamishe kuwa sisi tunafanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za sheria.
“Hivyo tunapoona jambo limezua mtafaruku huwa hatupendi kuliongea na hatutaki kabisa kuliongelea suala hilo kwa sababu tunaogopa mvurugano wa kitaasisi, kama mwandishi una roho ya kuleta amani kwenye jamii mkilizungumzia litaleta reaction za aina mbalimbali. Kwa mantiki hiyo sisi Takukuru hatuna ‘comment’ yoyote ya kuzungumzia hilo suala, nakuomba unielewe kwa nia njema. Kama ni uchunguzi tunaomba mtuachie sisi ili uonekane baada ya siku lakini kwa sasa tusiseme lolote,” alisema Misalaba.
TUHUMA ZA MAKONDA
Makonda aliwatuhumu Kamishna Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba huenda wanapokea rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa kikundi cha wafanyabiashara 10 wa kilevi cha shisha, waliomshauri azichukue yeye kila mwisho wa mwezi ili waendelee kufanya biashara hiyo, lakini alikataa kwa kile alichodai kuwa walikuwa ni mawakala wa shetani.
Alisema kwamba, kutokana na rushwa hiyo ndiyo maana Sirro na Kaganda wanalegalega kuwakamata wafanyabiashara hao waliomfuata ofisini kwake, licha ya kuwaagiza kufanya hivyo.
Licha ya Makonda kutoa tuhuma hizo, lakini Majaliwa alimtaka kufuatilia maagizo aliyowapa kina Sirro na asipofanya hivyo atamwajibisha kwa kushindwa kusimamia maagizo yanayotolewa na viongozi wa juu serikalini, ikiwamo kupiga marufuku biashara ya shisha jijini Dar es Salaam.
Kutokana na tuhuma za kina Sirro kuibua mjadala, Makonda aliendelea kuzizungumzia katika kipindi cha Power Break Fast, kilichorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM, kwa lengo la kutoa ufafanuzi zaidi na alisema anashangaa kuona vyombo vya habari vikizungumzia zaidi kauli yake badala ya kuelimisha madhara ya shisha.
“Nilifikiri watu wote wenye fikra pana wana wajibu wa kutafuta madhara ya shisha kuliko kuhangaika na kauli ambayo madhara yake hayapo. Tulikuwa na maadhimisho ya watoto njiti duniani na moja ya sababu zinazosababisha watoto hao ni utumiaji wa shisha, nilifikiri ningeona vyombo vya habari vimelizungumzia hilo, lakini hakuna kilichofanya hivyo,” alisema.
Pia alipoulizwa kwanini hakuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara 10 waliotaka kumpa rushwa, Makonda, alisema si kila hatua inayochukuliwa inasemwa.
“Haujui hatua zinazochukuliwa, si kila hatua inasemwa. Ukifanya jambo kama hili maana yake unatangaza katika namna mbili, kwanza unaongeza awareness (uelewa) kwamba hawa watu si kwamba wanafanya biashara ya shisha kwa sababu ni biashara, bali wanatafuta faida kwa nguvu yoyote, hata ya kukuangamiza wewe unayekwenda kutumia,” alisema Makonda.
JIBU LA SIRRO
Wakati Makonda akisema hayo, kwa upande wake Kamishna Sirro naye akahojiwa kipindi cha Sunrise kinachorushwa na Kituo cha Redio Times Fm cha Dar es Salaam, ambapo alimtaka Makonda achukue hatua kulingana na nafasi aliyonayo ya Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Dar es Salaam, kama atakuwa na wasiwasi na utendaji wa polisi katika operesheni ya kuondoa wafanyabiashara wa kilevi hicho.
“Mkuu wa Mkoa ana wasiwasi, huo ni wasiwasi na ubaki kuwa wasiwasi, kikubwa niseme sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, yeye ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama na kama atakuwa na wasiwasi na chombo chake najua atatuita na kutuambia nini cha kufanya, lakini kama ana wasiwasi zaidi yeye ni kiongozi, atajua achukue hatua gani dhidi ya sisi,” alisema Sirro.
Pia alisema operesheni ya kutokomeza shisha jijini Dar es Salaam inaendelea na hadi sasa watu waliokamatwa ni wengi na taratibu zinafanyika ili kuweza kuwafikisha mahakamani.
“Kinachofanyika lazima jalada lipelekwe kwa wakili wa Serikali ili kuandaa mashtaka na kupeleka mahakamani, kazi inafanyika, labda kama tutacheleweshwa na masuala ya ushahidi,” alisema Sirro.
Kuhusu wafanyabiashara 10 wa shisha waliotaka kumpa rushwa Makonda ili kumziba mdomo, alisema hawezi kusema chochote katika hilo. “Mkuu wa Mkoa ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama, aseme yeye alipeleka wapi? Maana vitu vingine ni siri, siwezi kumsemea kama alipeleka wapi, ukimaliza kuongea na mimi mtafute umuulize alipeleka wapi anaweza akakujibu,” alisema Sirro.