23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MBIVU, MBICHI CC YA CCM LEO

mfuko2

NA MWANDISHI WETU – dar es salaam

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inaanza vikao vyake leo, ikiwa ni mwanzo wa safari ya saa 72 ya mabadiliko makubwa ya kiuongozi ndani ya chama hicho.

Vikao hivyo vinavyofanyika leo na kesho na kufuatiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao utafanyika kesho, vinatarajiwa kuleta sura mpya za wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ambayo huzaa sekretarieti ya chama hicho chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

Tayari joto la mabadiliko limetawala hisia za makada wa CCM, huku majina ya wanasiasa wakubwa yakitajwa kutoka na mapya kuingia ndani ya CC.

Hisia za mabadiliko hayo zinachochewa na uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Magufuli kuwateua watu wenye nafasi nyeti za uongozi ndani ya chama hicho kushika nafasi mbalimbali za kiserikali.

Uamuzi wake wa kuwateua Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana na kabla ya hapo Dk. Asha Rose Migiro ambao wote ni wajumbe wa CC kuwa mabalozi, inatajwa kuwa msingi na chachu ya kutokea kwa mabadiliko.

Aidha, hatua ya kumteua Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kunatajwa pia kuwa mwelekeo wa kuingia kwa sura mpya katika nafasi nyingine kadhaa ndani ya vikao vya sekretarieti na CC ya chama hicho.

Taarifa mpya ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza kuwa masuala ya kifedha kwa maana ya madeni na matumizi ya fedha za chama zilizotumiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, nayo yanaweza kuchochea wimbi la mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama hicho.

Hivi karibuni, mfanyabiashara, Erick Shigongo aliandika andiko refu kupitia vyombo vyake vya habari, akiilaumu CCM kwa kushindwa kumlipa deni lake kwa kuchapisha fulana na kofia za chama hicho.

Inaelezwa kuwa Shigongo ni miongoni wa watu kadhaa waliopata kufanya biashara na CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao wanakidai fedha nyingi chama hicho.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata, lakini hazijaweza kuthibitishwa mara moja na viongozi wa CCM kutokana na kutopatikana, ni kwamba chama hicho kinadaiwa zaidi ya Sh bil. 48 zilizotokana na kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Wataalamu wa sayansi ya siasa wanaamini katika njia mbili za kufanya mabadiliko, kwanza ni kuwaweka mbali na ngome yako wale wote ambao unahisi huwahitaji au watakusumbua huko uendako, pili ni kuwaweka karibu sana na kuwadhibiti haswa. Haya ndiyo tunayaona mwenyekiti atayafanya, na upo uwezekano wa kuzaliwa kwa CC mpya kabisa,” alisema mtoa taarifa wetu.

Miongoni mwa mabadiliko yanayotarajiwa kutokea ni yale yatakayogusa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara) iliyokuwa ikishikiliwa na Luhwavi.

Mbali ya hilo, upo uwezekano wa Mwenyekiti Magufuli kutumia fursa hiyo kuwateua watu wapya kuongoza idara za chama hicho, ambazo wakuu wake wamepewa majukumu mapya ya kiserikali.

Gazeti dada la hili  la MTANZANIA Jumamosi jana liliripoti kuwa miongoni mwa idara zitakazoguswa na mabadiliko hayo ni ile ya Mambo ya Nje iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Migiro na ile ya Uenezi na Itikadi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Pia hatua ya Rais Magufuli kuwateua Luhwavi, Nchimbi, Pindi na kabla ya hapo Dk. Migiro katika nafasi za ubalozi, upo uwezekano mkubwa kwa wateule hao wapya kutangaza kujiuzulu nafasi zao za ujumbe wa CC ndani ya chama hicho tawala leo au kesho.

Iwapo hilo litatokea, mambo mawili yanaweza yakaandamana na uamuzi wao huo, la kwanza likiwa ni kwa Mwenyekiti Magufuli kujaza nafasi zao na wa pili ukiwa ni kuondoka kwa wajumbe wengine wote wa Kamati Kuu kama ilivyopata kutokea miaka minne iliyopita.

Wajumbe wanaounda Kamati Kuu ya CCM kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge, Job Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Wengine ni Luhwavi, Vuai Ali Vuai, Nape, Muhammed Seif Khatibu, Zakhia Meghji, Migiro, Sophia Simba, Sadifa Juma Khamis, Abdallah Bulembo, Jenister Mhagama, William Lukuvi, Steven Wasira, Nchimbi, Chana na Jerry Slaa.

Wamo pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Dk. Salim Ahmed Salim, Makame Mbarawa, Hadija Abood, Adam Kimbisa, Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Mwinyi na Maua Daftari.

Miongoni mwa majina yanayotajwa kuingia katika Kamati Kuu ni lile la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi.

Mbali na hayo, nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho inayoshikiliwa na Kinana ndiyo inayoonekana kupandisha zaidi joto hilo.

Taarifa kutoka ndani ya CCM zinadai kuwa ni mapema kusema iwapo Kinana ambaye katika miaka ya hivi karibuni amekuwa nguzo muhimu ya utendaji, anaweza kuondolewa katika nafasi hiyo, kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa ndani unaokikabili chama hicho mwakani.

Pamoja na kwamba zipo taarifa zinazodai kuwa upo uwezekano mkubwa wa Makamu Mwenyekiti CCM- Bara, Phillip Mangula, mwanasiasa anayetajwa kuwa karibu zaidi kiimani machoni mwa Dk. Magufuli na Kinana kuendelea kubaki katika nafasi hiyo, taarifa nyingine zinadai kuwa Katibu Mkuu huyo anakabiliwa na changamoto ya madeni na mapungufu mbalimbali ya uendeshaji wa vyombo vya habari vya chama hicho.

Septemba 22 mwaka huu, bodi nzima ya Uhuru Publication iliandika barua ya kujiuzulu, ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za magazeti ya chama hicho na kusikiliza kero za wafanyakazi, ambao walikuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi kadhaa, huku menejimenti ikidai kwamba inadai ofisi nyingi za Serikali, jambo ambalo kiongozi huyo aliahidi kulishughulikia haraka.

Hata hivyo, wakati Kinana akipewa nafasi ya kuendelea kushikilia wadhifa huo, taarifa nyingine zinamtaja mwanasiasa kijana, Mwigulu Nchemba kuwa mtu anayeweza kubebeshwa mikoba ya ukatibu mkuu wa CCM.

Mwigulu, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho wakati Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete alipokuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.

Mbali na Mwigulu, jina la Abdallah Bulembo nalo limeanza kutajwa katika nafasi za kiuongozi ndani ya chama hicho.

Kuwapo kwa hisia za kufanyika kwa mabadiliko katika Kamati Kuu na kwa wakuu wa idara wanaounda sekretarieti, kumeonekana kuwavuruga baadhi ya wana-CCM ambao wanaonekana kuyahofia mabadiliko hayo.

Julai 23, mwaka huu, wakati Rais Magufuli alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, alimwomba Kinana na sekretarieti nzima ya chama hicho kuendelea kukitumikia hadi hapo yatakapofanyika mabadiliko mengine.

Ingawa hakusema atafanya lini mabadiliko ya sekretarieti yake, lakini Rais Magufuli aliwashtua wale waliokuwa wana ndoto ya kumrithi Kinana kwa kuwaambia kuwa “wamenoa”.

Vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakuwa ni vya kwanza tangu Rais Magufuli achaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Kufanyika kwa kikao cha NEC jijini Dar es Salaam na si Dodoma kama ilivyozoeleka, kumeelezwa na baadhi ya wana-CCM kuwa kunatoa ishara ya kufanyika kwa jambo kubwa ndani ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles