25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

LEMA AANDIKA BARUA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)

Na AGATHA CHARLES – Dar Es Salaam

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye yuko mahabusu katika Gereza Kuu la Kisongo, jijini Arusha, amemwandikia barua wakili wake John Mallya, akimtakia heri katika ndoa yake na mkewe Neema Swai iliyofungwa jana.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na mkuu wa gereza, Lema alisema alitamani kuungana na Mallya katika tukio hilo lililofanyika jijini Arusha, lakini alishindwa kutokana na sheria kutoruhusu.

Lema alisema akiwa jela anapata nafasi ya kuomba kwa bidii hali ambayo anaamini inamfurahisha mno Mwenyezi Mungu.

“Natamani sana kuwepo, namwomba Mungu niwepo, lakini naona nikuandikie ujumbe ufuatao; John kama kuna jambo muhimu ambalo sijawahi kujutia katika maisha yangu ni kuoa. Ndoa ni baraka, Biblia inasema apataye mke amepata kitu chema, nashukuru Mungu kwa sababu umepata kitu chema,” alisema Lema.

Lema alimweleza Mallya kuwa wapo vijana wengi ambao wanaishi maisha ya ubatili katika ndoa zao, lakini si kwa sababu shetani ana nguvu bali kutokana na kupuuza maagizo na sheria za Mungu katika maisha yao.

Aliwaasa maharusi hao kwamba hawawezi kuwa na maisha bora na ya maana ikiwa Mungu hatokuwa sehemu yao ya kwanza kwa kila kitu, na kuwa familia bora inajengwa kwa kumcha Mungu hasa katika ulimwengu huu uliojaa majaribu.

Lema katika barua hiyo alisema alitamani kula keki, kuona maharusi hao namna walivyovaa na kupendeza, lakini ilishindikana na hivyo huko jela alipata nafasi ya kuwaombea.

“Ninawaombea sana kwani huku jela nina nafasi sana ya kuomba kwa kweli, naomba mpaka Mungu anafurahi. John kama jela wangeniamini wangenipa tu ruhusa nije halafu Jumapili nirudi zangu jela, sasa hawawezi kuniamini, kuniruhusu hata kidogo, eti sheria hairuhusu,” alisema.

Katika barua hiyo, pia Lema alimweleza wakili wake huyo namna wanavyofungiwa mapema, huku akimsimulia kisa kilichotokea baada ya yeye kulala saa 12 jioni.

“John huku jela tunawahi sana kufungiwa, leo (jana) niliwahi sana kulala, saa 12 jioni nilikuwa nimesinzia, nikastuka usingizini na kuanza kupiga mswaki kumbe ni saa nne usiku, nikacheka kidogo mwenyewe, basi kwa vile nilikuwa nimepanga kukuandikia wewe na Mhe. Sumaye (Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema) ndio sasa nafanya kazi hiyo,” alisema Lema.

Pamoja na salamu za barua hiyo, Lema pia alimtumia Mallya kadi iliyochorwa na kijana mmoja gerezani, huku akimtaka kuitunza kwa kuwa haipatikani sehemu yoyote isipokuwa gerezani.

Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa Lema anashikiliwa katika Gereza Kuu la Kisongo, jijini Arusha baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma.

Alifikishwa mahakamani jijini Arusha, Novemba 8, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles