27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, BILIONEA DANGOTE WAKATA MZIZI WA FITINA

Rais Dk. John Magufuli akisalimiana na mmiliki wa Kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote, Ikulu Dar es Salaam jana walipokutana na kufanya mazungumzo.
Rais Dk. John Magufuli akisalimiana na mmiliki wa Kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote, Ikulu Dar es Salaam jana walipokutana na kufanya mazungumzo.

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

HATIMAYE mzozo ulioibuka baada ya Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichoko Mtwara kusitisha uzalishaji, umemkutanisha mmiliki wake, bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote na Rais Dk. John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam jana.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu kupitia Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Jaffar Haniu, katika mazungumzo yao, Rais Magufuli ameibua hoja mpya ambazo aghalab hazijapata kuripotiwa ama na maofisa wa Serikali au wale wa bilionea huyo tangu kuibuka kwa mzozo huo yapata wiki moja iliyopita.

Rais Magufuli alisema hapakuwa na tatizo lolote kuhusu kiwanda hicho, isipokuwa mradi huo uliingiliwa na wapiga dili.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho Serikali yake hairuhusu.

Pasipo kufafanua kwa undani wala kumtaja yeyote, Rais Magufuli alisema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji yake, wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote zaidi ya watu hao kujitengenezea faida.

Rais Magufuli alimuhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa Serikali yake itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya viwanda.

Alisisitiza kuwa ujanja waliotaka kufanya watu hao hauwezekani katika Serikali yake.

“’Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha, uwasiliane na viongozi wa Serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili,” Rais Magufuli alimwambia Dangote.

Hatua ya kiwanda cha Dangote kinachokadiriwa kuajiri wafanyakazi 10,000 kusitisha uzalishaji kwa kile ilichoeleza kuwa ni hitilafu za kiufundi, imeibua sintofahamu ambayo kwa wiki moja habari zinazogusa tukio hilo zilitawala vichwa vya habari vya magazeti na mijadala mikali katika mitandao ya kijamii.

Dangote, tajiri anayekadiriwa kuwa na ukwasi unaofikia thamani ya dola za Marekani bilioni 14.9, amewekeza kiasi cha dola milioni 500 katika kiwanda hicho cha saruji.

Hatua ya kiwanda hicho kusitisha uzalishaji iliwaibua mawaziri wa Nishati na Madini, Profesa Peter Muhongo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), wote wakikishutumu kwa kutaka kununua gesi kwa gharama ndogo jambo walilosema haliwezekani na kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya nchi kinyume na makubaliano ya kutumia yale ya hapa nchini.

Katika hilo, Rais Magufuli alimtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha Serikali, badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.

Kwa upande wake, Dangote alidai kushangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania, kitu ambacho alisema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.

Mfanyabiashara huyo alisema ameingiza malori mapya 600 ya kusambazia saruji yake.

Katika kuthibitisha hilo, muda mfupi baada ya Ikulu kusambaza taarifa ya Dangote kukutana na Rais Magufuli, meli kubwa ambayo haijapata kutia nanga katika bandari ya Mtwara, jana ilipakua magari hayo.

Yeye mwenyewe akizungumza Ikulu, alisema lengo lake la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida, pia ni kuisaidia Serikali ya Tanzania kutengeneza ajira, hivyo hana sababu ya kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.

Bilionea huyo ambaye amewekeza katika nchi mbalimbali duniani, alimuhuhakikishia Rais Magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda chake.

Zaidi alisema ana mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kukutana kwa Rais Magufuli na Dangote kumekuja wakati ambao mzozo huo ulionekana kuvuka mipaka ya nchi na kuibua mambo mengi mpya ambayo hata hiyo katika taarifa ya Ikulu haikuonyesha kama yeyote kati yao aliyazungumzia.

Jarida maarufu linalofuatilia nyendo za kibiashara za watu wenye ukwasi mkubwa duniani, akiwamo Dangote, wiki iliyopita liliripoti juu ya tukio hilo, huku likiibua baadhi ya hoja.

Forbes katika taarifa yake hiyo, likinukuu kile ilichokiita taarifa za Serikali, lilidai kuwa uamuzi huo wa menejimenti ya Dangote kusitisha uzalishaji, umetokana na kuongezeka kwa gharama kubwa za uendeshaji.

Sababu nyingine ambayo ilitajwa katika jarida hilo kupitia tovuti yake, ni kile ilichodai ‘kutozingatiwa kwa makubaliano ya mkataba’.

Forbes ilitaja sababu nyingine ya kusitishwa kwa uzalishaji wa kiwanda hicho kuwa ni hatua ya Serikali kusitisha uamuzi wa kuiondolea Dangote ushuru wa forodha katika mafuta ya dizeli ambayo imekuwa ikiyaingiza nchini kuendeshea mitambo yake.

Kwa mujibu wa Forbes, kiwanda hicho kiliomba TPDC kusaidiwa upatikanaji wa gesi asilia kwa bei nafuu, lakini maombi yao yalikataliwa.

Wakati Forbes wakiripoti hayo, TPDC katika taarifa yake iliyotolewa katikati ya mzozo huo, ilisema kiwanda hicho kilikuwa kikitaka kuuziwa gesi kwa bei ya chini mno.

Kwa mujibu wa TPDC, kiwanda hicho kimeomba kupewa gesi asilia kwa bei ambayo hapa nchini ndiyo inayolipwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.

TPDC ilisema haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani, kwa sababu kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kusafirisha.

Katika andiko lake, Forbes ilieleza kuwa kiwanda hicho kinatumia kiasi cha dola milioni nne, sawa na Sh bilioni 8.7 kila mwezi kwa kununua mafuta ya dizeli ili kupata nishati ya umeme kuzalishia saruji.

Forbes walikwenda mbali na kukariri kile kinachodaiwa kuzungumzwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Dangote, Harpeet Duggal, mbele ya kundi la wanasiasa, Oktoba mwaka huu akisema; “Kiwanda chetu kinatumia lita milioni sita za dizeli kwa mwezi ili kuwezesha uzalishaji wa umeme kupitia jenereta, baada ya ahadi za kupatiwa gesi asilia inayozalishwa karibu na kiwanda chetu kutotekelezwa.”

Mbali na hayo, jarida hilo la Forbes lilibainisha kile kinachoeleza namna Serikali ya awamu ya nne ya Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na ya awamu ya tano ya Rais Magufuli zilivyochukua hatua zinazotofautiana juu ya mkataba wa kiwanda cha Dangote.

Jarida hilo lilimkariri ofisa mmoja wa Kampuni ya Dangote, ambaye alikataa kutaja jina lake kwa kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia sakata hilo, akisema kufungwa kwa kiwanda hicho kutawalazimu maofisa wa Serikali kurudi kwenye makubaliano ya msingi yaliyofikiwa kati yake na kiwanda hicho.

Forbes linaeleza katika taarifa yake hiyo kwamba; “chini ya uongozi wa Kikwete, maofisa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), walimpatia Dangote ahadi ya nafuu ya kodi na nyingine zisizotajwa.”

Forbes pia ilihusisha uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa TIC, Juliet Kairuki, Aprili mwaka huu na sakata hilo la Dangote, jambo jipya na ambalo halijapata kutajwa tangu kuibuka kwa sakata hilo.

Hata hivyo, jarida hilo la Forbes linakiri kwamba Ofisi ya Rais haikupata kubainisha sababu za kufutwa kazi kwa mkurugenzi huyo.

Wakati Forbes wakilihusisha tukio la Kairuki na sakata la Dangote, taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, ilisema pamoja na mambo mengine, hatua hiyo ilichukuliwa na Rais Magufuli baada ya kupata taarifa kuwa mkurugenzi huyo alikuwa hachukui mshahara wa Serikali tangu alipoajiriwa mwaka 2013, jambo lililozua maswali.

Kuhusu makaa ya mawe, Forbes limedai kuwa uamuzi wa Serikali kupiga marufuku ununuzi wa nishati hiyo nje ya nchi, ulikilenga pia kiwanda cha Dangote.

Forbes katika taarifa yake imerejea kutaja mzozo juu ya ubora na gharama za makaa ya mawe kati ya yale yanayozalishwa hapa nchini na yale kutoka nchini Afrika Kusini, ambako Kampuni ya Dangote imekuwa ikiyaagiza.

WAAPISHWA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amuapisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher ole Sendeka anayechukua nafasi ya Dk. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Wengine walioapishwa ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (Kilimo), Dk. Maria Sasabo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Dk. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Grace Martin kuwa Balozi (Mkuu wa Itifaki).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles