25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

BEKI WA CHAPECOENSE APATA NAFUU NCHINI COLOMBIA

3b26493d00000578-0-image-a-41_1481144635458

RIONEGRA, COLOMBIA

BEKI wa klabu ya soka ya Chapecoense, Alan Ruschel, ambaye amenusurika na kifo katika ajali ya ndege iliyotokea wiki moja iliyopita na kuua wachezaji 19 wa klabu hiyo, amepata nafuu na kuongea kwa mara ya kwanza kwa mashabiki wake.

Ruschel, mwenye umri wa miaka 27, alikuwa miongoni mwa watu 82 waliopata ajali hiyo, huku watu 71 wakipoteza maisha papo hapo, lakini yeye alitoka salama na kukimbizwa katika hospitali ya Somer Clinic iliyopo nchini Colombia.

Timu ya Chapecoense ilikuwa inaelekea nchini Colombia kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa fainali za kombe la Copa Sudamericana, ambapo walitakiwa kucheza na timu ya nchini hapo,  Atletico Nacional.

Hata hivyo, Atletico Nacional, ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo, walitoa ombi kwa Shirikisho la Soka Amerika Kusini kwamba ubingwa wa michuano hiyo wapewe Chapecoense kwa heshima yao na shirikisho hilo lilikubali ombi hilo na kuwapa ubingwa mapema wiki hii.

Ruschel amewashukuru mashabiki wote wa soka na wadau mbalimbali kwa dua zao za kumuombea aweze kupona mapema.

“Namshukuru kila mmoja, namshukuru kila mmoja ambaye ameguswa na tukio zima na wale wote ambao walikuwa wananiombea kwa ajili ya kutaka nirudi katika hali ya awali, mimi ni Alan Ruschel.

“Nataka kuwaambia kwamba kwa sasa ninaendelea vizuri na ninaamini muda mfupi ujao nitarudi nchini Brazil kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

“Nawashukuru wote kwa dua zenu pamoja na sapoti yenu kwa njia ya ujumbe wa maandishi ambao nimeupata kutoka kwenu, asanteni sana.”

Daktari wa mchezaji huyo ambaye anaendelea kumhudumia katika hospitali hiyo, Marcos Sonagli, amedai kuwa, mchezaji huyo hana tatizo kubwa katika afya yake, awali walidhani kuwa atakuwa na tatizo la kuvunjika kwa mgongo.

“Ruschel anaendelea vizuri na matibabu yanaendelea, awali alionekana kuwa katika hali mbaya kutokana na kusumbuliwa na mgongo, wala hakuvunjika na sasa anaendelea vizuri na hata kutembea anaweza,” alisema Sonagli.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Klabu ya Chapecoense, Ivan Tozzo, amevishukuru vyama mbalimbali vya soka pamoja na Shirikisho la Soka nchini Brazil, CBF, Shirikisho la Soka America Kusini (CONMEBOL), pamoja na Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, kwa mchango wao katika kipindi hiki kigumu kwa klabu hiyo.

“Tunashukuru kwa vyama vyote ambavyo vimekuwa pamoja nasi kwa kipindi hiki kigumu, wadau wa soka na mashabiki wamekuwa pamoja nasi, tunawashukuru sana, kwa sasa tupo katika kupambana kwa ajili ya kuijenga timu, tunaamini watu wanapenda mpira hapa Chapeco, hivyo lazima tupambane ili kuweza kuendelea kuwa na timu, hasa msimu ujao,” alisema Tozzo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles