27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

SAA 72 ZA MABADILIKO CCM

kinana

Na MWANDISHI WETU

WAKATI vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikitarajiwa kuanza kuketi ndani ya saa 24 zijazo jijini Dar es Salaam, joto la mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama hicho limepanda na kufikia kiwango cha juu.

Kuwapo kwa mabadiliko hayo kunachagizwa na uamuzi wa hivi karibuni kabisa wa Rais Dk. John Magufuli kuwateua watu wenye nafasi nyeti za uongozi ndani ya chama hicho kushika nafasi mbalimbali za kiserikali.

Uamuzi wake wa kuwateua Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana na kabla ya hapo Dk. Asha Rose Migiro ambao wote ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kuwa mabalozi, inatajwa kuwa msingi na chachu ya kutokea kwa mabadiliko.

Aidha, hatua ya kumteua Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kunatajwa pia kuwa hatua nyingine inayochagiza kuingia kwa sura mpya katika nafasi nyingine kadhaa ndani ya vikao vya sekretarieti na kamati kuu vya chama hicho.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya CCM, zinaeleza kuwa, baada ya kamati kuu kumaliza kikao chake cha siku mbili keshokutwa, uko uwezekano wa kutokea kwa mabadiliko makubwa yanatarajiwa kutangazwa Jumanne katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).

Miongoni mwa mabadiliko yanayotarajiwa kutokea ni yale yatakayogusa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara) iliyokuwa ikishikiliwa na Luhwavi.

Mbali ya hilo, upo uwezekano wa Mwenyekiti Magufuli kutumia fursa hiyo kuwateua watu wapya kuongoza idara za chama hicho ambazo wakuu wake wamepewa majukumu mapya ya kiserikali.

Miongoni mwa idara hizo ni ile ya mambo ya nje iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Migiro na ile uenezi na itikadi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Baadhi ya makada wa muda mrefu wa CCM wamelieleza gazeti hili kwamba, hatua ya Rais kuwateua Luhwavi, Nchimbi, Pindi Chana na kabla ya hapo Dk. Migiro katika nafasi za ubalozi, upo uwezekano mkubwa kwa wateule hao wapya kutangaza kujiuzulu nafasi zao za ujumbe wa CC ndani ya chama hicho tawala.

Iwapo hilo litatokea, mambo mawili yanaweza yakaandamana na uamuzi wao huo, la kwanza likiwa ni kwa Mwenyekiti Magufuli kujaza nafasi zao na wa pili ukiwa ni kuondoka kwa wajumbe wengine wote wa Kamati Kuu kama ilivyopata kutokea miaka minne iliyopita.

Wajumbe wanaounda Kamati Kuu ya CCM kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula.

Wengine ni Katibu Mkuu wa CCM,Abdulrahman Kinana.

Wamo pia, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Wengine ni Luhwavi, Vuai Ali Vuai, Nnauye, Muhammed Seif Khatibu, Zakhia Meghji, Asha Rose Migiro, Sophia Simba, Sadifa Juma Khamis, Abdallah Bulembo.

Wengine ni Jenister Mhagama, William Lukuvi, Steven Wasira, Nchimbi, Chana, Jerry Slaa, Adam Kimbisa, Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Mwinyi na Maua Daftari.

Wapo pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Dk. Salim Ahmed Salim, Makame Mbarawa na Hadija Abood.

Miongoni mwa majina yanayotajwa kuingia katika Kamati Kuu ni lile la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi.

Mbali na hayo, nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho inayoshikiliwa na Kinana ndiyo inayoonekana kupandisha zaidi joto hilo.

Taarifa kutoka ndani ya CCM zinadai kuwa, ni mapema kusema iwapo Kinana ambaye katika miaka ya hivi karibuni amekuwa nguzo muhimu ya utendani anaweza kuondolewa katika nafasi hiyo, kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa ndani unaokikabili chama hicho mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, upo uwezekano mkubwa wa Kinana kuendelea kubaki katika nafasi hiyo pamoja na Makamu Mwenyekiti CCM- Bara, Phillip Mangula, mwanasiasa anayetajwa kuwa karibu zaidi kiimani machoni mwa Dk. Magufuli.

Viongozi hao wawili wakongwe katika chama hicho, wanapewa nafasi kubwa ya kuendelea na nyadhifa zao ili kuweza kukiongoza chama hicho kuelekea katika mabadiliko kamili makubwa mwakani.

Hata hivyo, wakati Kinana akipewa nafasi ya kuendelea kushikilia wadhifa huo, taarifa nyingine zinamtaja mwanasiasa kijana, Mwigulu Nchemba kuwa mtu anayeweza kubebeshwa mikoba ya ukatibu mkuu wa CCM.

Mwigulu, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho wakati Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete alipokuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.

Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM kililieleza gazeti hili kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli, anayo nafasi kubwa ya kutumia vikao hivyo kuunda Kamati Kuu mpya ambayo itazaa sekretarieti mpya ya chama hicho.

Kuwapo kwa hisia za kufanyika kwa mabadiliko katika kamati kuu na kwa wakuu wa idara wanaounda sekretarieti kumeonekana kuwavuruga baadhi ya wana-CCM ambao wanaonekana kuyahofia mabadiliko hayo.

“Hapa ndipo joto linapoanzia, si unajua mwenyekiti alivyo msiri, watu hawaelewi kama viongozi wa sasa wataendelea au watawekwa pembeni,” alisema mtoa habari mmoja.

Katika hatua nyingine, duru zaidi kutoka ndani ya CCM zinadai kwamba, joto hilo la mabadiliko limeibua kundi la moja la watu wenye ushawishi kuhofia hatua zozote ambazo zinaweza kumuondoa Katibu Mkuu, Kinana.

Kundi hilo linadaiwa kujenga ushawishi wa kutaka Kinana aendelee na wadhifa alionao au nafasi yake ishikwe na mtu mwingine mwenye kukifahamu vyema chama hicho.

Kundi hilo linadaiwa kumtaja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwa mtu pekee wanayemuona kuwa na uwezo wa kuvaa viatu vya Kinana.

Julai 23, mwaka huu, wakati Rais Magufuli alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, alimuomba Kinana na sekretarieti nzima ya chama hicho kuendelea kukitumikia hadi hapo yatakapofanyika mabadiliko mengine.

Ingawa hakusema atafanya lini mabadiliko ya sekretarieti yake, lakini Rais Magufuli aliwashtua wale waliokuwa wana ndoto ya kumrithi Kinana kwa kuwaambia kuwa “wamenoa”.

Vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ambavyo vitafanyika hivi karibuni vitakuwa ni vikao vya kwanza tangu Rais Magufuli achaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Kufanyika kwa kikao cha NEC jijini Dar es Salaam na si Dodoma kama ilivyozoeleka, kumeelezwa na baadhi ya wana-CCM kuwa kunatoa ishara ya kufanyika kwa jambo kubwa ndani ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles