Na DORINE OTINGA, NAIROBI
KUNA yepi mekoni? Jungu la kisiasa linazidi kuchemka. Mvuke unaonekana kwa umbali. Palipo na moshi hapakosi moto eti. Naam, namna uchaguzi unavyokaribia nchini Kenya, ndivyo joto la kisiasa linavyozidi kutanda nchini.
Kila mwanasiasa anajaribu kusafisha na kutengeneza njia yake kwa manufaa ya siku zijazo. Upinzani unazidi kutoa sera zake huku upande mwingine ukijaribu kutoa sera nzuri zaidi.
Ni hali ya lala salama katika pande zote mbili, huku kila mmoja akijaribu kufanya afanyalo, kisha liwe liwalo. Wananchi wanazidi kutumbua macho na kuangalia ni yupi atakayefaa. Japo pande zote zina mvuto kivyake, itakuwa jukumu la kila mmoja kuamua ni nani atakayeongoza Kenya tokea 2017.
Naibu wa Rais Ruto ana lipi mekoni?
Naibu wa Rais William Ruto ana umaarufu sana, hasa katika Mkoa wa Bonde la Ufa (Rift Valley) hapa Kenya. Katika miaka kumi iliyopita amethibitisha umaarufu wake kwa kupata nyadhifa mbalimbali katika Serikali.
Baada ya kujiunga na chama cha Jubilee ambacho Rais Uhuru Kenyatta ndiye nahodha wake, bado alizidi kupata umaarufu, licha ya sakata kuu iliyokuwa ikimkumba ya kuwa na kesi katika mahakama ya ICC.
Ruto anakipigia debe chama cha Jubilee kipate kushinda tena katika uchaguzi wa 2017. Aidha, ana imani kwamba mwaka wa 2022 atachukua fursa ya kusimamia kiti cha urais baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongoza kwa awamu mbili, iwapo atashinda katika uchaguzi ujao. Rutto ametoa hotuba katika vikao mbalimbali vya kisiasa, huku akihudhuria hafla za kuchangia fedha katika sehemu mbalimbali, kama vile makanisani na shule mbalimbali pia.
Mwezi uliopita alizuru eneo la Pwani. Alisema kwamba hakuwa huko katika ziara za kikazi tu, bali alikuwa akijiandaa katika uchaguzi wa 2017 na 2022.
“Ingawa tumetoka sehemu mbalimbali kisiasa, nina imani kwamba wakati utakapofika mtaunga mkono uwaniaji wangu,” alisema Rutto.
Azma kuu ya William Rutto ni kupata mamlaka zaidi katika chama cha Jubilee, kutokana na magavana wengi na wabunge watakaoteuliwa kutoka katika upande wake. Hii itaongeza nguvu za ushawishi wake kutoka katika Chama cha Jubilee. Rutto anataka kuwa na mamlaka dhidi ya kaunti mbalimbali. Analenga angalau Kaunti 20 na wabunge 120.
Kwingineko, kizaazaa kilizuka katika maskani ya Boma Inn, katika Kaunti ya Nyeri ambako kulikuwa na mkutano ambao uliongozwa na kundi la kumpigia kampeni Rais Uhuru na baadhi ya wagombea katika timu ya chama cha Jubilee walizusha mtafaruku huku wakimwambia Gavana Nderitu Gachagua ambaye ni msimamizi wa kundi hilo kwamba walitaka kuongezwa katika kundi hilo.
Madai ya wagombea wasiokuwepo kundini ni kumtaka Gavana huyo awaongeze au waondoke katika Chama cha Jubilee. Kulitokea na ubishi mkali ambao ulisababisha vita baina yao, huku wakirushiana mateke. Wengine walitaka suala la kundi hilo la kukampeni kuzungumziwa kwanza, huku wengine wakitaka wakubaliane kwanza jinsi uteuzi baina yao utakavyofanywa.
Ziara za Rais Uhuru Kenyata
Uhuru Kenyatta kwa upande wake anafanya kila juhudi kuhakikisha kura za urais 2017, zinamwangukia bila shaka. Mnamo Novemba 28, mwaka huu aliwatembelea Wamachinga wa Nyeri katika kituo chao cha biashara cha Chaka. Alizindua miradi yenye thamani ya shilingi milioni 13 akiwa na Naibu wake, William Ruto.
Kando na hayo, alizusha malalamishi yake dhidi ya kiongozi wa upinzani wa chama cha Cord, Raila Odinga. Uhuru alisema kiongozi huyu anafanya siasa za kijinga ambazo zinafanya nchi kuwa dhaifu. Naye Rutto alilaumu vyombo vya habari kwa kukubali kutumiwa na upinzani kupanda mbegu za chuki nchini. Rais Uhuru Kenyatta alimwomba Raila Odinga kujiuzulu katika siasa na kuwachia vijana wadogo.
“Labda ni umri wake unaofanya tumwombe ajiuzulu sasa manake ni mzee mkongwe. Tutahakikisha kwamba amehudumiwa vizuri. Kama kawaida, nitamletea sahani ya uji huko Bondo kama ataondoka,” alisema Rais Uhuru.
Patashika za Raila Odinga
Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa asiyechoka na mwenye wingi wa juhudi hapa nchini Kenya, anazidi kujikakamua kupambana na Jubilee. Licha ya kuwania kiti cha urais mara tatu na kushindwa, bado anayo ari ya kuwa rais.
“Mara nyingi nilishinda katika uchaguzi, lakini nilitolewa nje,” alisema Raila, alipozungumzia na jarida la Newsweek la London.
Mwaka wa 2017, Raila anapanga kuwania kiti hiki tena. Wakati huu, kiongozi huyu wa upinzani anapanga kuondoa vizuizi vyote vile vitakavyomzuia kuingia ikulu. Mapema Mei mwaka huu Odinga aliongoza maandamano ili kuiondoa IEBC ambayo chama cha ODM hakikuwa na imani nayo.
Hii ilikuwa njia moja ya kuondoa vizuizi ambavyo anadhani vitamzuia kupata kiti cha urais mwaka wa 2017. Kwa upande mwingine, upinzani unaonekana kutimiza malengo yake. Kwake Odinga, mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi (IEBC) ni ya maana ili kuzuia machafuko kama ya mwaka 2007.
Raila alimkashifu Rais Uhuru Kenyata kutokana na kutochukua hatua yoyote dhidi ya viongozi wakuu ambao wanashukiwa kuhusika na fedha zilizopotea katika kashfa ya NYS. Imekuwa jukumu la kiongozi huyu kukashifu makosa mbalimbali ambayo aliyaona katika serikali ya Kenyatta.
Wakenya wanazidi kutarajia kwamba mwaka wa 2017 watamchagua kiongozi anayefaa. Japo maoni wa kila Mkenya hayafanani, ni matumaini ya kila mmoja kwamba amani itadumishwa.
Kwa maoni +254 716955356