NA ZAINAB IDDY,
KOCHA mwenye maneno mengi nchini, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema bado hajafikiria kurejea mapema kwenye kazi hiyo kutokana na kuchoshwa na tabia mbovu za waamuzi wa mchezo huo.
Kocha huyo wa zamani wa Mwadui ya Shinyanga na mchezaji wa Simba, alisema pamoja na baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuhitaji huduma yake, lakini bado hajaamua kufanya hivyo kwa sababu hajaridhishwa na maendeleo ya mchezo huo kwa sasa.
“Zipo baadhi ya timu zimenifuata kutaka nikazifundishe, nazishukuru kwa kutambua uwezo wangu, lakini sipo tayari kufanya hivyo kwa sasa, haya ni maamuzi yangu binafsi, waniache nitekeleze kile ninachoona sahihi.
“Soka la hapa nchini ni gumu, nimevumilia kwa kipindi kirefu lakini kutokana na hali iliyopo kwa sasa ni bora nikae pembeni na kuwapisha wengine waendelee,” alisema Kihwelo.
Alisema anachojivunia katika ufundishaji wake ni ubora na mafanikio kwenye baadhi ya timu alizowahi kuzifundisha, ikiwemo kuipandisha daraja timu ya Mwadui karibu misimu miwili iliyopita na kumaliza nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.
Jamhuri Kihwelo ni miongoni mwa makocha wazuri katika soka la Tanzania waliowahi kufundisha timu mbalimbali za Ligi Kuu pamoja na ile ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, 20 na 23 kwa mafanikio makubwa.
Kocha huyo aliamua kujiuzulu kufundisha soka la Tanzania akiwa na kikosi cha Mwadui kutokana na kile alichodai waamuzi wa mchezo huo wameshindwa kutafsiri sheria 17 za soka.