Na MANENO SELANYIKA-
DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeendelea kusikiliza mashahidi katika kesi ya ndugu wanaogombea sehemu ya kumzika marehemu Ernest Kalegu, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Mwili huo umekwama kuzikwa kwa siku ya 14 sasa kwa sababu mdogo wa marehemu, mke na mtoto wanabishana wapi mwili huo ukazikwe.
Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Thomas Simba wa mahakama hiyo, huku upande wa mdaiwa unasimamiwa na Wakili Magaki Masatu na upande wa wadai ukiongozwa na Wakili Raymond Wawa.
Akitoa ushahidi jana, mtoto wa marehemu, Edwin, alieleza kuwa Novemba 24, mwaka huu, baba yao alitakiwa awe ameagwa na wafanyakazi wenzake aliokuwa anafanya nao kazi, kwa hiyo hakukuwa na tarehe rasmi ya kuaga mwili kwa kuwa kulikuwa na watu muhimu ambao hawakufika.
Kwa upande wake, mjane wa marehemu, Dyana Willy, alidai marehemu ni mumewe na alifunga naye ndoa Mei 12, 1970 katika Kanisa Katoliki lililopo Chang’ombe, jijini Dar es Salaam na alizaa naye watoto wanne ambao ni Joyce, Irene, Edwin na Rita na alikuwa akiishi naye Dar es Salaam na Nairobi na kuhusu taratibu za mazishi ilipaswa aulizwe kwamba mumewe azikwe wapi.
Alidai kwamba mtu wa kwanza kumpigia simu alikuwa shemeji yake aitwaye Pius na siku hiyo alikuwa Nairobi, nchini Kenya.
“Kipindi chote nikiwa Nairobi nilikuwa nikiwasiliana na mume wangu kwa njia ya simu. Wakati nilipopigiwa simu hiyo niliambiwa mwili wa marehemu ndio unaingizwa mochwari Muhimbili. Nikiwa katika taratibu za safari niliambiwa mwili unasafirishwa Novemba 24, mwaka huu,” alidai Dyana na kuongeza:
“Niliwauliza kwanini wamsafirishe wakati mwenyewe alisema kati ya yeye au mimi tukifa tuzikwe Dar es Salaam na kutokana na hatua hiyo hakukuwa na maelewano ya simu kuhusu hatua hiyo.
“Nilifika Jumamosi Novemba 26, mwaka huu saa sita usiku na nilipofika nikasikitishwa na taarifa kwamba mwili ulikuwa umeshasafirishwa kwenda Bunda.”
Hata hivyo, wadaiwa waliuliza baba wa marehemu alipozikwa na mjane huyo alijibu kuwa alizikwa Ngorembe, Bunda na alipewa habari hizo na mama mkwe.
Pia alidai kuwa hakuwahi kutengana na mumewe.
Wakili Masatu aliendelea kumuuliza kuwa kwa ushahidi uliopo ni kwamba Agosti 25, 2009, mumewe alifungua kesi Mahakama ya Mwanzo Temeke kwa ajili ya kuvunja ndoa. Lakini Dyana alimjibu kuwa hata yeye alishangaa kuiona barua hiyo na kabla ya mumewe kufariki alikuwa akiishi Ukonga na alikuwa akiongea naye mara kwa mara.
Naye mtoto wa nne wa marehemu, Rita, alidai kuwa alipata taarifa za msiba Novemba 20, mwaka huu na alifika usiku wa Novemba 24, mwaka huu.
“Nilipofika uwanja wa ndege nikitokea Marekani nilipokelewa na ndugu na marafiki. Baada ya kunipokea wakaniambia tayari mwili wa baba upo njiani unasafirishwa kuelekea Bunda na niliambiwa umechukuliwa na baba mdogo,” alidai Rita na kuongeza:
“Nilikwenda Marekani tangu Septemba, 2001 na nilirudi Tanzania mwaka 2004, kisha baba alikuja mwaka 2005 na mimi nilirudi tena mwaka 2006. Mara ya mwisho kuonana na baba ilikuwa mwaka 2014.
“Kuhusu taarifa za kifo nilipewa na shemeji yangu na dada yangu kwa njia ya simu na ujumbe wa maneno.”
Shahidi wa tano ambaye ni baba mdogo, Gonche Materego, alidai kwamba marehemu alimuacha mke wake kwa talaka iliyotolewa na Mahakama ya Mwanzo Temeke.