25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU BURE IAMBATANE NA MAZINGIRA BORA

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


 

Mkurugenzi-mtendaji-wa-twaweza-aidan-eyakuze
Mkurugenzi-mtendaji-wa-twaweza-aidan-eyakuze

UTAFITI uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Twaweza unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wazazi wenye watoto wanaosoma shule za msingi wa

napenda watoto wao wasome katika shule binafsi ukilinganisha na walio tayari kuwapeleka katika shule za umma.

Utafiti huo unaonyesha asilimia 60 ya Watanzania wanapenda watoto wao wasome katika shule binafsi na asilimia 36 shule za umma huku asilimia tatu wakisema wanapenda aina zote za shule.

Utafiti huo uliopewa jina la ‘Uwezo’ ulilenga kupima ubora wa elimu tangu kuanza kutekelezwa kwa sera ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema hiyo ni ishara tosha kuwa wananchi wana mashaka na ubora wa elimu inayotolewa katika shule za serikali kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Wananchi waliotaja elimu bora ni asilimia 45, uwapo wa walimu wanaofanya kazi kwa bidii na wanaopewa motisha (12), idadi ya kutosha ya walimu (12) kama sababu kuu za kuzipendelea shule binafsi,” anasema Eyakuze.

Anasema asilimia 50 walisema ubora wa elimu nchini umeongezeka tangu kuanzishwa kwa sera ya elimu bure wakati asilimia 35 walisema ubora huo umebaki palepale huku asilimia 15 wakisema umeshuka.

Anasema katika moja ya shule zilizoko Mbagala yako malalamiko ya idadi kubwa ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza tofauti na matarajio ambapo walitegemea kuandikisha wanafunzi 300 lakini wakaandikishwa zaidi ya 1,000.

Ofisa Miradi wa Shirika hilo, Nellin Njovu, anasema kuwa asilimia 90 ya wazazi wenye watoto wa shule za msingi watoto wao wanasoma katika shule za umma, asilimia sita wanasoma shule binafsi na asilimia nne katika shule za umma na binafsi.

Ili kuhakikisha kiwango cha elimu kinaimarishwa serikali inapaswa kuhakikisha inaongeza nguvu katika kuboresha elimu kwa kuweka mazingira bora.

Kuwe na vyumba vya madarasa vya kutosha vilivyo na madawati yatakayomwezesha kila mwanafunzi kuketi vizuri sambamba na upatikanaji wa vitabu angalau kufikia wastani wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili.

Makazi na masilahi bora kwa walimu si jambo la kupuuzwa ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji kwani si rahisi kwa mfanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa anaishi katika mazingira yasiyoridhisha.

Ikiwa mtu anakabiliwa na matatizo katika familia yake yanayogusa maisha yake moja kwa moja ni wazi kuwa hataweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Utafiti huo pia umebaini mambo yanayochangia kushuka kiwango cha elimu kwa wanafunzi ni makundi rika asilimia 16, umaskini (14), mimba za utotoni (12), kazi za nyumbani (9), kukosa chakula (7), matumizi ya dawa za kulevya (6), ajira za utoto (6), unyanyasaji dhidi ya watoto (5) na ndoa za utotoni (4).

Ukosefu wa vyoo na huduma zingine muhimu ni mingoni mwa mambo yanayozikabili shule za umma kwa kukosa uwiano baina ya idadi ya wanafunzi na matundu ya vyoo.

“Wasichana 125 hutumia tundu moja kinyume cha sera ya elimu ya mwaka 2014 inayotaka tundu moja kutumiwa na wasichana 20 hii ikiwa ni mara sita zaidi ya kiwango kinachotakiwa.

“Wavulana 130 hutumia tundu moja badala ya 25 kwa tundu moja kama sera inavyoelekeza kuwa tundu moja litumiwe na watoto 25,” inasomeka sehemu ya utafiti huo.

Ukosefu wa vitabu pia ni moja ya mambo yaliyoonyeshwa katika utafiti huo ambapo katika mkoa wa Mara wanafunzi 126 wa shule ya msingi hutumia kitabu kimoja, Pwani 56 wakati Mtwara, Njombe, Ruvuma, Katavi na Kilimanjaro wanafunzi watatu hutumia kitabu kimoja.

Hii inaonyesha kuwapo kwa mahitaji makubwa ya vitabu katika shule zote za umma ili kuongeza ufanisi kwani si rahisi mwanafunzi kujifunza na kuelewa vizuri hasa katika mazingira ambayo yana uhaba wa vitabu.

Kama serikali ilivyoihamasisha jamii kuchangia upatikanaji wa madawati kupitia halmashauri zake inapaswa kufanya hivyo kuwezesha upatikanaji wa vitabu vya kutosha.

Pia kiwango cha elimu kimekuwa kikiathiriwa na wazazi au walezi kutojihusisha na maendeleo ya elimu ya watoto wao.

Jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiathiri maendeleo ya watoto kutokana na kutokuwa na hofu ya kufuatiliwa na wazazi pale wanapofanya makosa iwe kutohudhuria vipindi ama kutofanya majaribio yanayotolewa shuleni.

Japo wengi wanaweza wasilione hili kama tatizo lakini tunapaswa kukubaliana kwa pamoja kuwa mzazi kufuatilia maendeleo ya shule ya mwanawe ni suala lisiloepukika ikiwa anategemea kupata matokeo chanya kwa mtoto wake.

Pia ni vema suala la elimu likatenganishwa na siasa na kutotafsiri tofauti kauli za watendaji na viongozi wa serikali.

Kwa mfano utekelezaji wa elimu bure umeibua mitazamo ambayo si mizuri, ambapo baadhi ya jamii wamekataa kuchangia gharama ambazo zinastahili kuchangiwa kwa madai kuwa serikali iliahidi kutoa elimu bure.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles