24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

DC ANAYEPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA ELIMU NKASI

Na Khamis Mkotya, aliyekuwa Rukwa


mkuu-wa-wilaya-ya-nkasi-said-mtanda“NIMEKUTA wilaya ina upungufu wa madawati 5,000 kwa kushirikiana na wananchi tumemaliza tatizo hilo bila michango ya mashirika wala makampuni kama ilivyo kwa wilaya za mijini.

“Nilitangaza kila kijiji kitengeneze madawati na ndani ya kipindi cha miezi mitatu tumefanikiwa kutengeneza madawati 550 kwa nguvu za wananchi wenyewe.

“Pia nimekuta shule za msingi zina upungufu wa vyumba vya madarasa 1,150 kwani shule zote zina vyumba 650 tu wakati mahitaji ni 1,800.

“Nimehamasisha kila kijiji kiwe na benki ya matofali ili kujenga madarasa mapya, nawashukuru wananchi kwa kuniunga mkono, hadi sasa tunayo matofali 500,000,”.

Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, wakati akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake hivi karibuni kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili wilaya hiyo iliyopo mkoani Rukwa.

Nkasi inapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika, ina kata 30, vijiji 105 na majimbo mawili ya uchaguzi, Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini.

Mtanda anasema Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa wilaya zilizopo pembezoni zenye changamoto nyingi za kielimu.

Anasema baada ya kuwasili wilayani humo alifanya ziara vijijini, ambapo alibaini wilaya hiyo ina changamoto kubwa ya miundombinu hasa kwa upande wa sekta ya elimu.

Anasema licha ya wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1979, lakini miundombinu yake ni hafifu hali inayosababisha tatizo la msongamano wa wanafunzi, kutokana na uhaba wa madarasa.

Anasema tatizo hilo limekuwa kubwa mwaka huu baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza sera ya elimu bure, ambapo wazazi wengi wamehamasika kupeleka watoto wao shule.

“Kwanza namshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuniamini na kuniteua mimi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, ninachotaka kumuahidi tutafanya yale ambayo yeye anayatarajia.

“Mimi kama mkuu wa wilaya ni mwakilishi wa Rais lazima tufanane na Rais na kufanana na si kwa sura bali kwa matendo na tabia zile ambazo mheshimiwa Rais anazo.

“Ni tabia zile za kiuongozi, kuchukia rushwa, kuwahudumia wananchi kwa wakati, kufanya mikutano ya vijijini lakini pia kubana matumizi.

“Wilaya hii ilianzishwa mwaka 1979 mkuu wa wilaya wa kwanza alikuwa akiitwa Bakari Kipanga na baadae akaja mkuu wa wilaya anaitwa Iddy Mapinda na wengine, mimi ni mkuu wa wilaya wa tisa hapa Nkasi.

“Wilaya hii ina tarafa nne ambazo ni Chala, Namanyere na tarafa nyingine mbili zipo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, Tarafa ya Wampembe na Tarafa ya Kirando. Tarafa hizi jirani zao ni Kongo na mahusiano yao ni wananchi wa Kigoma wanakuja sana kupitia Ziwa Tanganyika.

“Katika miezi minne kati ya vijiji 105 nimeshatembea vijiji 50 hivyo tayari nusu ya wilaya hii naifahamu, nimehamasisha katika sekta za kilimo, ufugaji, maji, afya, elimu na uvuvi,” anasema.

Akizungumzia sekta ya elimu, Mtanda anasema katika elimu ya msingi kuna changamoto nyingi zinazotishia kukwamisha elimu wilayani humo, tofauti na upande wa sekondari ambako kuna unafuu kitaaluma.

“Tumeamua kuimarisha elimu ya msingi maana huko ndiko kwenye matatizo makubwa. Mkakati wa kwanza ni kuhakikisha kila shule inakuwa na madawati ya kutosha.

“Hadi sasa tumeshatengeneza madawati 5,000 ambayo ndiyo yalikuwa pungufu na kazi ya kusambaza inaendelea kwenye shule mbalimbali,” anasema.

“Mkuu wa wilaya aliyepita alitengeneza madawati 2,000, mimi nilipokuja nilikuta upungufu 3,000 tuliweka nguvu kazi mimi na wafungwa tulikwenda porini kukata magogo.

“Tulipata magogo zaidi ya 1,500 tukachana mbao wenyewe tukapa mbao zaidi ya 6,000 tukatengeneza madawati, lakini tukanunua vyuma vya kutengeneza madawati mengine kama 2,000.

“Tumeokoa fedha nyingi kwa kutengeneza madawati kwa mbao tu na misumari. Kwa hiyo nusu ya madawati tumetengeneza kwa chuma na nusu kwa mbao.

“Tatizo jingine ni uhaba wa vyumba vya madarasa, tuna vyumba 650 wakati mahitaji ni 1,800, tuna wanafunzi 68,000 kwa hiyo utaona tuna upungufu mkubwa sana wa madarasa.

“Hatua gani tumechukua, kwanza hadi sasa tumeshajenga maboma 38 katika mkakati wetu wa benki ya matofali kila kijiji kina matofali 20,000 hadi 30,000 vipo vingine vina tofali hadi 100,000

“Hadi sasa katika benki yetu tuna matofali 500,000 kwa vijiji vyote na kazi hiyo imefanyika Oktoba na Novemba.

“Ili kumaliza tatizo la vyumba tunahitaji kuwa na matofali 1,100,000 hapa tunavyozungumza nusu yake tunayo.

“Wananchi wengine wameshaanza kukusanya mchanga na mawe wajibu wa Serikali ni kupeleka saruji, mbao na mabati kwa ajili ya kupaua.

“Fedha tunazo Sh milioni 148 kwa ajili ya kununua vifaa hivyo, kijiji kitakachoonyesha madarasa matatu tunawapa saruji, nondo, mbao na mabati.

“Tumejipa malengo kwa miezi mitatu hadi Februari mwakani tutaongeza vyumba vitatu vya madarasa kila shule, hivyo tutaongeza vyumba 315 rekodi ambayo hakuna wilaya nchini wataifikia zaidi ya Nkasi,” anasema.

Anasema baada ya Februari mwakani, atahakikisha vyumba vingine 500 vinajengwa ili kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mkuu huyo wa wilaya anasema sera ya elimu bure imeleta changamoto zaidi, kwani wazazi wengi wamepata mwamko wa kupeleka watoto wao shule na hivyo tatizo la upungu wa madarasa likaendelea kuwa kubwa.

“Tunaishukuru Serikali kwa sababu watoto wengi sasa wanapata elimu, lakini ni changamoto kwa sababu ni lazima tuongeze madawati na vyumba vya madarasa, ndiyo maana tumejipanga hadi Februari mwakani, tuwe tumeongeza madarasa mengi,” anasema.

Mapato

Kuhusu pato la Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Mtanda anasema; “Nikiwa mkuu wa wilaya hapa nimefanya ziara saa nane usiku zaidi ya mara nne kwenye mageti na nimekamata magari zaidi ya matano, tumeongeza mapato kwa sasa tunakusanya hadi Sh milioni 175 kwa mwezi.

“Huko nyuma halmashauri ilikuwa inatumia mawakala kukusanya mapato walikuwa wanapata milioni 59, lakini kuanzia Julai hadi Novemba mwaka huu tunakusanya kati ya Sh milioni 175 hadi 200,” anasema.

Mtanda anasema pamoja na mapato hayo kutumika kuendeshea halmashauri, lakini kiwango kingine kinatengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, jambo ambalo linaloifanya wilaya hiyo izidi kupata mafanikio.

Kwa upande wa sekta ya afya, Mtanda anasema amelazimika kuchukua baadhi ya hatua na kutoa maagizo kadhaa kwa wakuu wa idara na vijiji mbalimbali ili kuboresha huduma za afya.

“Katika sekta ya afya tunachokisimamia sasa hivi kwanza ni kumaliza miundombinu ya afya kwa mfano zahanati nimekuta baadhi ya zahanati zimejengwa hazijapauliwa.

“Jambo la pili ni upatikanaji wa dawa, unafika kijijini unakuta wanakijiji wanafedha kwenye akaunti, lakini zahanati hazina dawa.

“Tulichofanya ni kuagiza serikali za vijiji na kamati za afya za vijiji fedha isikae kwenye akaunti badala yake inunue dawa, kama MSD (Bohari Kuu ya Dawa) hawana dawa tuwape kibali wanunue dawa kwenye maduka binafsi,” anasema.

Mbali ya tatizo la dawa, Mtanda anasema tatizo jingine katika sekta hiyo ni uzembe wa madaktari katika Hospitali ya Wilaya ya NDDH iliyopo Namanyere, lakini amefanikiwa kupunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.

CWT

Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Nkasi, kimempongeza Mtanda kwa namna anavyoshirikiana na chama hicho katika kushughulikia na kutatua kero za elimu wilayani humo.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake, Katibu wa CWT, Aurea Mwanakulya, anasema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini wanaamini zitakwisha chini ya uongozi wa mkuu huyo wa wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles