Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
 ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na makosa ya kushindwa kuhifadhi silaha wamekutwa wana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai mahakamani kwamba wateja wake watajitetea wenyewe pamoja na mashahidi watatu ambapo jumla watakuwa na mashahidi saba.
Hakimu Mkeha alisema washtakiwa wataanza kujitetea Desemba 13 mwaka huu.
Mbali na Gwajima wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kwa kukutwa wakiwa na begi lililokuwa na vitu mbalimbali ikiwamo risasi 17 na bastola ni Askofu Msaidizi, Yekonia Bihagaze , mfanyabiashara George Mzava na Mkazi wa Kimara Baruti Geofrey Milulu.
Wanadaiwa kukutwa na vitu hivyo katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni chumba namba 213 alipokuwa amelazwa Askofu Gwajima.
Inadaiwa Machi 29, 2015, saa 9 usiku watu watatu ambao ni mshtakiwa wa pili hadi wa nne walifika hospitalini hapo huku mmoja wao akiburuza begi la kijani hadi karibu ya mlango wa kuingilia katika wodi aliyolazwa Gwajima.