Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM
KOCHA mpya wa timu ya Yanga, George Lwandamina, ameweka wazi juu ya hatima ya mwanandinga ndani ya Yanga kwa kuahidi kuzungumza nao ili wabaki iwapo ataridhishwa na viwango vyao.
Uamuzi huo unatokana na kuwepo kwa minong’ono ya straika wa kimataifa wa klabu hiyo, Mzambia Donald Ngoma na kiungo Vincent Bossou, kugomea kuongeza mkataba mpya baada ya kupata dili la kwenda kucheza timu nyingine.
Ngoma na Bossou walijiunga na Yanga kwa mikataba ya miaka miwili kila mmoja na hivi sasa kandarasi zao zinataraji kumalizika mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu huu.
Kutokana na kubaki miezi michache kabla ya kuvunjia ndoa zao na Yanga, mabosi wa klabu hiyo walipanga kuwapa mikataba mipya ya miaka miwili, lakini inadaiwa wanandinga hao wamegoma kutokana na kupata ofa nyingine nono kutoka klabu ya Mamelod Sundown ya Afrika ya Kusini kwa Ngoma, huku Bossou akidaiwa kupata dili Misri, kwenye klabu ya Zamalek.
Taarifa ambazo MTANZANIA limezipata kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa licha ya kocha wao mpya, Lwandamina kuangalia viwango vya wachezaji wote kupitia CD, ameweza kuweka wazi juu ya kuzungumza na Ngoma kama ataridhishwa na kiwango chake mara baada ya kukutana naye.
“Baada ya kuangalia CD na kutoa tathmini ya mchezaji mmoja mmoja, alipewa taarifa za Ngoma pamoja na Bossou kutaka kuondoka kutokana na ofa walizozipata, kocha ameahidi kuzungumza nao ili wabaki, lakini kama ataridhishwa na viwango vyao.
“Kocha amesema hawezi kubariki kuondoka kwao ikiwa hajawaona, hivyo atakapokutana nao kwenye mazoezi ndipo atatoa maamuzi juu yao na wengine, lakini kama watakuwa na ubora anaouhitaji atahakikisha anatumia mbinu zake za ukocha kuwashawishi ili waweze kuendelea kuitumikia Yanga kwa misimu mingine tena,” alisema.
MTANZANIA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, kujua ukweli wa habari hiyo, ambapo alisema kwa siku za hivi karibuni hawataachana na mchezaji yoyote hadi pale kocha wao, Lwandamina atakapobariki suala hilo baada ya kukutana na wachezaji.
“Timu inaingia kambini hivi karibuni kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi pamoja na mashindano mengine, kocha ametutaka kutoachana na mchezaji yeyote hadi pale atakapokutana nao na kuona uwezo wao, hivyo yanayozungumzwa yapo mikononi mwake, kwani hata hivyo, muda wa usajili bado haujafungwa, lakini pia wachezaji wanaozungumza tuna mkataba nao bado,” alisema.