Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania imebaini wizi wa Sh bilioni tatu zilizokuwa zikisainiwa na kuchukuliwa kwa ajili ya mafuta ya magari mabovu yasiyotembea.
Shirika hilo pia linaidai Serikali Sh bilioni 7.3 na taasisi binafsi Sh bilioni 1.9 kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwamo upangaji wa majengo ya shirika hilo.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Harun Kondo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkataba wa utendaji kati ya bodi hiyo na Mtendaji Mkuu wa Shirika.
Dk. Kondo alisema tatizo lililokuwapo katika shirika hilo ni ubadhirifu.
Alisema wapo wafanyakazi walikuwa wakisaini fedha, zikafikia Sh bilioni tatu wakidai ni kwa ajili ya mafuta ya magari wakati magari hayo yote mabovu na hayatembei.
“Shilingi bilioni tatu hazieleweki zilipo. Walikuwa wanasaini fedha zinatolewa kwa ajili ya mafuta ya magari, magari yenyewe mabovu hayatembei.
“Hawa wahusika watambuliwe, wachukuliwe hatua, kama watasimamishwa au kufukuzwa kabisa.
“Hakuna maelezo ya fedha hizo, huu ni wizi, wahusika wanajulikana lazima hatua zichukuliwe.
“Mikataba mibovu tulikubaliana ije, tuliagiza haijaja, tarehe 13 tutakaa kuipitia iletwe, hasara ni kubwa watu wanasaini mikataba ya gharama ndogo na shirika halipati kitu.
“Tutafanya upekuzi, tukishindwa wenyewe tutaita hata watu wa nje waje kufanya upekuzi,”alisema.
Mtendaji Mkuu, Fortunatus Kapinga, alibainisha mikataba mibovu kuwa ni miwili ambako mmoja ni uwanja uliopo jirani na Ubungo Plaza na jengo la ghorofa sita lilipo Ubungo Mawasiliano.
Kapinga akizungumzia madeni ambayo shirika hilo linadai, alisema wanaidai Serikali Sh bilioni 7.3 na taasisi binafsi Sh bilioni 1.9 kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwamo upangaji wa majengo ya shirika hilo.
Akizungumzia mabadiliko, Dk. Kondo alisema katika kuhakikisha yanakuwapo maendeleo, shirika limejipanga kutekeleza majukumu kwa kufuata dira, shirika liende na mabadiliko ya sayansi, liende na kasi ya ushindani wa biashara.
“Tutafikia kupeleka barua mpaka nyumbani, tutakuwa na utaratibu wa kuondoa urasimu pamoja na viashiria vya rushwa, tumekubaliana kuyafanya haya, bodi inaingia mkataba wa sheria kuyatekeleza.
“Mkataba tutakaoingia utasainiwa kati ya Mwenyekiti wa bodi na Mtendaji Mkuu kisha Mtendaji Mkuu naye anasaini mkataba mwingine na watendaji,”alisema na kuongeza kwamba watapeana muda wa utekelezaji.
Mkataba huo wa utendaji unatarajiwa kusainiwa Desemba 13 mwaka huu.
Alisema baada ya hatua hiyo bodi itakuwa ikifuatilia utekelezaji.