Na Christian Bwaya
KATIKA makala iliyopita tuliona kuwa mwanamke anahitaji kujua anavyopendwa na mwenzi wake kwa maneno na vitendo. Mwanamke anatamani kusikia kwa maneno na kuona kwa vitendo kuwa anapendwa.
Kwa wanaume wengi mambo haya hayana maana, kwao kama unampenda mkeo na unajua ni kweli unampenda si lazima kufanya juhudi endelevu za kumthibitishia kuwa unampenda. Lakini kwa wanawake kuambiwa wanapendwa huburudisha moyo wa mwanamke.
Katika makala haya tunatazama mahitaji mengine mawili aliyonayo mwanamke.
Anataka kuwa kipaumbele chako
Mwanamke hapendi kujikuta katika mazingira ya kushindania nafasi ya kwanza na kitu kingine chochote iwe ni kazi, mtu au chochote kile unachokipenda wewe mwanamume.
Tulishaona kuwa kwa mwanamume hadhi yake hutegemea zaidi namna uwezo wake unavyotambuliwa. Hali hiyo humfanya mwanamume atumie muda mwingi kufanya mambo yanayoweza kumpa heshima katika jamii. Inaweza kuwa kazi, biashara, mamlaka na namna zozote zile zinazomwongezea uwezo.
Lakini wakati anapotumia muda mwingi katika mambo hayo ni rahisi kuonekana ameyafanya mambo mengine kuwa ya muhimu kuliko uhusiano wake na mwenzi wake. Wanawake wengi hawapendi kujikuta katika hali hii. Hapa ndiko iliko tofauti.
Mwanamke hatamani kuwa kwenye nafasi ya ‘mengineyo, ziada, baadae au nikipata muda’. Unapomweka ‘akiba’ mwanamke hawezi kufurahia kwa sababu anatamani awe kipaumbele chako.
Mambo mengi huthibitisha kuwa umempa nafasi ya kwanza. Mfano kuwa na muda wa kuwa naye mara nyingi kadiri inavyowezekana, kuahirisha mambo mengine ya muhimu kwa ajili yake, kuwahi miadi unapoahidi kukutana naye, kuwasiliana naye kwa karibu na mambo kama hayo. Unaposhindwa kufanya hivyo mwanamke hupata ujumbe kuwa yeye ni mtu wa ziada baada ya mambo ya muhimu.
Kadhalika ili kumwambia yeye ni kipaumbele, mwanamke anatamani kila unapoongea naye akili yako yote iwe pamoja naye. Kuwa pamoja naye maana yake ni kuachana na vyote vinavyokuondolea uzingativu na kumsikiliza kwa makini.
Mwanamke anatamani unapozungumza naye ufuatilie anachokisema, umpe mrejesho kuwa unamwelewa na uonyeshe kuwa mwili, akili, hisia ziko pamoja naye kumsikiliza. Vinginevyo mwanamke anakuoana kama hujaweza kumpa nafasi yake anayoistahili.
Kueleweka kwa hisia zake
Tumekwisha kuona kuwa mwanamume kwa kawaida hutamani kupewa hadhi ya kuwa na sauti ya mwisho kwa kusikilizwa. Kwa mwanamke hadhi yake hutegemea hisia zake zinavyoeleweka kwa mwenzi wake. Jambo hili ni gumu kidogo kueleweka kwa wanaume wengi kwa sababu nitakayoieleza.
Kwa kawaida wanaume hutamani kutoa majibu kwa matatizo. Uwezo wa kuwa na majibu ni sehemu muhimu ya heshima ya mwanamume. Ndio maana mwanamke anapomfuata mume wake pengine ili kusikilizwa na kueleweka, mara moja akili ya mwanamume hufanya kazi ya kuchakata majibu haraka na kuyakabidhi kwa mwanamke. Uharaka wa majibu humjengea mwanamume hali ya kujiamini.
Hata hivyo si wakati wote mwanamke anapokuwa na neno la kusema, basi hutamani kupata majibu kama ambavyo akili ya mwanamume inaweza kufikiri. Mara nyingi mwanamke anapolalamika lengo lake huwa ni kutafuta utulivu wa kihisia tu basi.
Mwanamke anatamani awepo mtu anayemwamini, anayeweza kusikiliza hisia zake kwa dhati bila kujaribu kuhukumu, kupuuza au kuelekeza vile anavyopaswa kujisikia. Anatamani liwepo sikio linaloaminika kwa mwenzi wake linaloweza kusikia na kuelewa kile hasa kinachomsibu nafsini mwake.
Itaendelea.
Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Â Â 0754 870 815