Na SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM
MCHEZAJI wa gofu kutoka Arusha, Nuru Molel, juzi ameibuka bingwa katika mashindano ya gofu ya Kombe la Waitara, kipengele cha wachezaji wa kulipwa (Professionals) ambayo yalifanyika viwanja vya Lugalo, jijini Dar es Salaam.
Molel aliwashinda jumla ya wachezaji wa kimataifa 21 walioshiriki michuano hiyo, kwa gloss 71, huku nafasi ya pili ikimwendea John Loence pia wa Arusha, aliyeshinda kwa gloss 72.
Hassan Kabio wa Klabu ya Gymkhana Dar es Salaam alimaliza nafasi ya tatu baada ya kushinda kwa gloss 72, ambapo washindi walitarajiwa kukabidhiwa zawadi zao jana jioni.
Waitara Trophy iliendelea jana kwa kushirikisha vipengele vyingine, isipokuwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.
“Hakutakuwepo na ushiriki wa watoto wenye umri chini ya miaka 18 kutokana na mashindano haya kudhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti,” alinukuliwa nahodha wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Japhet Masai.
Waitara Trophy hufanyika kila mwaka, lengo ni kukumbuka mchango wa mwanzilishi wa Uwanja wa Gofu Lugalo, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Mstaafu George Waitara.