25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Milioni 60 kumbakiza Tshabalala Simba

mechi-3NA ASHA MUHAJI, DAR ES SALAAM

WEKUNDU wa Msimbazi ‘Simba’, wanatarajia kufanya yao kwa kumpa mkataba mnono wenye thamani ya Sh milioni 60 beki wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Tshabalala anatarajia kusaini mkataba mpya kesho baada ya kuitumikia Simba katika misimu mitatu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akitokea Kagera Sugar.

Mkataba wa awali wa mchezaji huyo uliodumu kwa miaka mitatu, ulikuwa una thamani ya Sh milioni 12,000, ambao kwa sasa una ongezeko la Sh milioni 48,000 katika mkataba mpya wa miaka miwili anaotarajia kusaini hiyo kesho.

Meneja wa mchezaji huyo, Heri Mzozo,  aliliambia MTANZANIA kuwa, masuala yote ya msingi kati ya pande hizo mbili wameyamaliza kwa asilimia 80, hivyo kusubiri kutia saini mkataba mpya.

Mzozo alisema kabla ya kufikia dau hilo, Simba walikuwa wametoa ofa ya Sh milioni 40, lakini kwa upande wao walisimamia dau la Sh milioni 60 ikiambatana na marupurupu kadhaa ambayo alikataa kuyaweka wazi kwa sasa.

Alisema akiwa ni meneja wa mchezaji huyo, ameamua kumbakisha Simba kutokana na umri wake kuwa bado mdogo, ili aendelee kukuza kipaji chake ndani ya klabu hiyo ambayo imeonekana dhahiri kama nyota yake iko huko.

“Kwa kweli ndani ya mkataba huu hakukuwa na matatizo japo inawezekana kama binadamu wakatofautiana kidogo,  isipokuwa msingi unabaki palepale kuwa alikuwa na maisha mazuri ndani ya timu hiyo na mimi sijaona sababu ya kumhangaisha mchezaji, tamaa pia si nzuri vema ukaheshimu utu,” alisema.

Akizungumzia sababu za kuingia mapema mkataba mpya ilihali ule wa zamani unamalizika Juni 2017, meneja huyo aliweka wazi ni kutaka kumaliza usumbufu ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa timu nyingine zikitaka kumweka sawa ili muda ukifika atie saini katika moja ya klabu hizo.

“Timu nyingi zilishaanza usumbufu, nami nafahamu wazi sheria, hatukuruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote kwa vile muda huo ulikuwa bado, hivyo ili kukata mzizi wa fitina nimeona bora tumalizane na mwajiri wake wa sasa, kwani bado anafurahia maisha ndani ya klabu hiyo.

“Ipo mifano ya wengi waliopotea stepu, hivyo sikutaka mchezaji wangu naye aje apotee kutokana na kuchanganywa katika vishawishi vinavyoweza kumfanya asicheze mpira. Tshabalala bado mdogo, ana uwezo pia umri unamruhusu kucheza muda mrefu hivyo ninataka atimize ndoto zake,” alisema.

Kusaini mkataba wa mchezaji huyo kutamaliza hofu iliyoanza kutawala miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo kama huenda angetimka na kuiacha kwenye mataa timu yake ambayo hivi sasa inapambana kutwaa ubingwa ilioukosa kwa misimu mitatu sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles