WANAFUNZI wa shule sekondari zaidi 300 wanaoishi Kata ya Ngemo wilayani Mbogwe katika Mkoa wa Geita wanakabiliwa na changamoto ya kutembea kilomita 20 kila siku kwenda masomoni katika shule ya sekondari Ushirika.
Diwani wa Kata hiyo, Lukas Sambayamoto alikuwa akizungumza  kwa masikitiko kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Alimuomba Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Elias Kayandabira kuifungua shule iliyoko katka kata yao.
Sambayamoto alisema  wazazi wamekwisha kujenga madarasa mawili,ofisi ya walimu,vyoo matundu manane  na maabara kwa nguvu zao ili kuwaondolea watoto wao adha hiyo.
Alisema   kata yake hiyo yenye vijiji saba, watoto wanapomaliza elimu ya msingi wanapochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, kila siku hutembea kilomita 20 kwenda shule yasekondari ya Ushirika.
Alisema hali hiyo husababisha utoro, mimba za utotoni na mdondoko mkubwa wa kutokumaliza shule.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbogwe, Elias Kayandabira, aliliomba baraza na diwani wa Ngemo wafanye subira ili naye aende akajiridhishe pamoja na wataalamu wa elimu kama shule hiyo ikikidhi vigezo   Januari mwakani itafunguliwa.
Kata ya Ngemo kwa muujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012, ina   watu 16,196,  kati ya hao wanawake ni 8,928 na wanaume 7,268.