Na TIMOTHY ITEMBE
SERIKALI imewaonywa wazee wa mila na wakazi wa Wilaya ya Tarime kuwa yeyote atakaebainika kukeketa mtoto wa kike atachukuliwa hatua kali.
Hatua hizo ni pamoja na kushtakiwa kwa kutenda ukatili ili liwe fundisho kwa wengine.
Onyo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga wakati akifungua semina ya siku moja iliyoandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) kwa udhamini wa Shirika la Faundation For Civil Socierty.
Luoga alisema kuendelea vitendo vya ukeketaji kumekuwa kukitokana na kutochukuliwa hatua wahusika.
Alionya kuwa sasa atasimamia kuhakikisha hatua zinachukuliwa vilivyo kukomesha jambo hilo ambao limekuwa likiharibu sifa ya wilaya hiyo kwa muda mrefu.
“Kila siku Serikali kwa kushirikiana na mashirika wamekuwa wakitoa elimu kwa wadau pamoja na wazee wa mila kuzuia na kukomesha ukeketaji.
“Sasa kwa kuwa huko nyuma kulilegalega sasa nawaeleza yeyote atakayebainika akimkeketa mtoto wa kike atachukuliwa hatua kali za sheria ikiwamo kukamatwa na kupandishwa mahakamani kujibu mashtaka,” alisisitiza.
DC alitumia fursa hiyo kuwataka wazee wa mila kusimamia mchakato wa kukomesha mila hiyo na kuwaasa wanajamii kuwapeleka watoto wa kiume kufanyiwa tohara hospitalini kitaalamu badala ya zile za kimila ambazo ni hatari kwa maisha ya watoto wao.
Mkurugenzi wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Coshuma Mtengeti, alisema kila watoto wawili waliochini ya umri wa miaka 18 mmoja kati yao anakeketwa.
Coshuma alisema lengo la mradi wa kukuza haki za mtoto wa kike ni kuutambulisha mradi, msimamo wa serikali kuhusu kukomesha ukeketaji kuwajengea uwezo wadau juu ya madhara ya ukeketaji.