UONGOZI wa klabu ya Atletico Madrid, wamekanusha taarifa kwamba mshambuliaji wao Nyota, Antoine Griezmann, kuwa amevunjika mfupa wa mguu, huku akiwa na timu yake ya taifa ya Ufaransa.
Mchezaji huyo kwa sasa yupo nchini Ufaransa akiwa na timu yake ya taifa kwa ajili ya michezo ya kufuzu Kombe la Dunia. Mchezaji huyo alipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, huku timu hiyo ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Sweden.
Griezmann hakumaliza mchezo huo baada ya kuumia katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, hivyo kukawa na taarifa kwamba mchezaji huyo amevunjika mguu.
Atletico Madrid wameweka wazi kuwa mchezaji huyo alipata maumivu lakini si kuvunjika mguu kama habari ambavyo zinaenea na mchezaji huyo atapata nafasi ya kucheza katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania dhidi ya watani wao wa jadi Real Madrid Jumamosi hii.
Atletico Madrid wamedai kuwa madaktari wanahakikisha mchezaji huyo anakuwa fiti kabla ya mchezo huo wa Jumamosi na inasemekana atakuwa mjini Madrid kwa ajili ya matibabu mbele ya jopo la madaktari.
“Kwa mujibu wa majibu ya x-ray ambayo alifanyiwa juzi, yapo wazi ni kwamba mchezaji huyo hajavunjika mguu lakini alipata matatizo ya misuli ya mguu.
“Habari zilienea kwamba mchezaji huyo amevunjika lakini huu ni ukweli ambao tunautoa kwa sasa, tunatarajia kumuona mchezaji huyo akiwa uwanjani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Jumamosi.
“Madaktari wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu hii wamekubaliana kwamba mchezaji huyo akafanyiwe matibabu mjini Madrid,” waliandika Atletico Madrid.
Hata hivyo, mchezaji huyo amewatoa wasiwasi mashabiki wa klabu hiyo kutokana na taarifa mbaya ambayo waliipata hapa awali na amewaahidi makubwa katika mchezo dhidi ya Real Madrid kwenye uwanja wa nyumbani wa Vicente Calderon.
“Haikuwa ajali mbaya kama watu wanavyodhani, kwa sasa ninaendelea vizuri na natakiwa kufanya mazoezi kutwa mara tatu kwa ajili ya kujiweka fiti kuelekea mchezo dhidi ya Real Madrid kwenye uwanja wa nyumbani, ninaamini kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Griezmann.
Katika msimu huu, mchezaji huyo amefanikiwa kuifungia klabu yake jumla ya mabao nane katika michuano yote aliyocheza, huku akitoa pasi za mwisho tano katika michezo 14 aliyocheza.