Na MWANDISHI WETU – GEITA
MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM), umetumia Sh milioni 750 kutengeneza madawati 10,000 ambayo yamekabidhiwa kwa uongozi wa Mkoa wa Geita ili yagawanywe katika wilaya tano za mkoa huo.
Akipokea madawati hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa jana, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi, alisema msaada huo utasaidia kumaliza tatizo kubwa la uhaba wa madawati.
“Tunapenda kushukuru mchango huu wa madawati, pia natambua jitihada nyingine za maendeleo zinazofanywa na mgodi wa GGM, ni jambo jema kuongeza misaada hii, mkoa wetu utaendelea kufanya vyema katika sekta ya elimu kwa kuwa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi umeanza kuimarika,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Apolinary, alisema mchango huo ni muhimu katika kuboresha elimu kwenye halmashauri hizo.
“Halmashauri ya Mji wa Geita ilikuwa na upungufu wa madawati 11,773, wakati yaliyopo ni 13,609, huku mahitaji yakiwa ni 25,190. Wilaya ya Geita ilikuwa na upungufu wa madawati 22,066, yaliyopo ni 33,514 na mahitaji ni 55,580.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Terry Mulpeter, alisema mgodi huo kama jirani mwema, umeguswa na upungufu wa madawati mkoani Geita na ndiyo sababu umeamua kuunga mkono jitihada za Serikali.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mseto, Grace Ndimuhele, alisema shule yake ina wanafunzi 1,266, lakini ina madawati 133, hivyo mchango wa GGM umekuwa mkombozi kwao.