33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Elimu usalama barabarani ianzie shule za msingi’

usalama-2Na HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM

MRATIBU wa bajaji na bodaboda wilayani Ilala, Renatus Nicholus, amesema ili kupunguza  ajali nyingi zinazotokea hivi sasa  vilabu vya elimu ya usalama barabarani ni muhimu kuanzishwa nchini kote  kuanzia shule za msingi ili  taifa la kesho liwe lenye vijana makini na watiifu katika sekta ya usafirishaji.

Aliyasema hayo juzi wakati  wa ufunguzi wa mashindano ya vilabu vya wanafunzi wanachama yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, ambavyo  vipo chini ya mpango wa utoaji elimu ya haki na wajibu wa mtumiaji mashuleni kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

“Kumekuwa na ajali nyingi  miaka kumi iliyopita nchini ambapo utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2007, unaonyesha kuwa asilimia 76 ya ajali zinazotokea zinatokana na makosa ya kibinadamu yakiwamo mwendokasi na uzembe, ndiyo maana kupitia mpango huu watoto wataweza kupata elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa usalalma barabarani na pia wataendelea kuwa mabalozi wazuri miaka ijayo,” alisema.

Aliongeza kuwa wanafunzi pia wamekuwa wakipata elimu juu ya kukabiliana na unyanyasaji wawapo kwenye vyombo vya usafiri na jinsi ya kuwa watii wa sheria za barabarani.

Shule ya Msingi Msimbazi iliibuka mshindi na kuzawadiwa Sh 100,000 ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Makongo iliyozawadiwa Sh 70,000 na Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa iliyojinyakulia shilingi 50,000, ilishika nafasi ya tatu. Washiriki walishindana katika kuonyesha sanaa mbalimbali za kuelimisha jamii juu ya usalama barabarani zikiwamo uigizaji, kwaya, ngoma za asili na mashairi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Washauri la Sumatra, Dk. Oscar Kikoyo, alisema walengwa wakuu ni wanafunzi kwa kuwa ndilo kundi ambalo bado lina damu changa na rahisi kuelimika.

Alisema mpango huo kwa sasa umeanzishwa katika mikoa nane ikiwemo Tanga, Dar es Salaam, Mwanza,  Arusha, Kagera, Kigoma, Mbeya, Mtwara na kwa sasa umeanza kutekelezwa mkoani Tabora.

Hadi sasa vimeanzishwa vilabu 2,300 katika mikoa hiyo ambapo mpango huo unategemea kuanzishwa katika shule zote nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles