Na Walter Mguluchuma, Mpanda
WAKAZI watatu wa kitongoji cha Senta ya Maradona katika Kijiji cha Kabange mkoani hapa, wamefariki dunia baada ya kunywa dawa waliyopewa na mganga wa kienyeji kutibu ugonjwa wa tumbo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alikiri kutokea tukio hilo na kuwataja marehemu hao kuwa ni Kabula Joseph (23) na Idulu Masanja (30) ambao ni wakwe wa mganga huyo.
Alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 13, mwaka huu nyumbani kwa mganga huyo, Msajigwa Jaheda (55).
Inaelezwa kuwa Mganga huyo alimpatia mke wa mtoto wake mdogo aitwaye Kabula dawa ya kienyeji ya kusafisha tumbo .
“Baada ya kutenda hayo mganga huyo alitoroka na kujificha kusikojulikana. Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kumtafuta mganga huyo,” alisema Kamanda Nyanda Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda, Dk. Mohamed Mpunja alisema baada ya kunywa dawa hiyo, Kabula alitapika na kupoteza nguvu mwilini na hatimaye alifariki dunia.
“Mtu mwingine aliyepoteza maisha ni Masanja ambaye alifika katika kitongoji hicho kuhani msiba.
“Kabla ya kurudi nyumbani kwake alienda kwa mganga huyo wa kienyeji aitibiwe tumbo la ngiri.
“Mganga huyo alimpatia dawa ambayo baada ya kuinywa alitapika na kuharisha na kisha alifariki dunia muda mfupi baadaye,” alisema.
Kutokana na tukio hilo, Dk. Mpunja amewataka wananchi mkoani humo kwenda kwenye vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa wowote ili kupata matibabu.