MAMLAKA ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (VETA), haijaajiri Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kwa takribani mwaka mmoja sasa.
Sababu ya kukosekana kwa mkurugenzi huyo ni kile kinachoelezwa kuwa mamlaka za juu kutothibitisha ajira ya mtu aliyeshinda usaili wa nafasi hiyo baada ya aliyekuwepo kusimamishwa kazi kabla hajastaafu kwa mujibu wa sheria.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya mamlaka hiyo, zimeeleza kuwa awali nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Aloyce Shayo ambaye alisimamishwa kazi na baadaye kustaafu.
Zimeeleza kuwa baada ya Shayo kustaafu Mwanasheria Mkuu VETA, Adeline Macha, ndiye aliyekaimu.
“Mwaka jana nafasi hiyo ilitangazwa watu wakaomba, wakafanyiwa usaili lakini hadi leo hii majibu hayajatolewa. Mambo yanaendeshwa kama hakuna ulazima wa kuwapo kwa mkurugenzi wa idara ya rasilimali watu.
“Unajua inashangaza, hata huyu aliyekaimishwa ingawa ana uwezo mkubwa wa kuongoza kitengo hicho lakini utaratibu unaelekeza kuwa ilitakiwa akaimishwe mtu anayetoka ndani ya kitengo husika.
“Anayekaimu sasa amebobea katika sheria na ndiye mkuu wa kitengo hicho hivyo kumpa akaimu ukurugenzi wa kitengo cha rasilimali watu ni kulazimisha,” alisema mmoja wa watoa taarifa ambaye jina lake tunalihifadhi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Geoffrey Sabuni, alipoulizwa kuhusu jambo hilo alikiri kuwa ni kweli mpaka sasa nafasi hiyo iko chini ya kaimu ambaye ni mkuu wa sheria.
Sabuni pia alikiri kuwa usaili ulikwishafanyika na mshindi alipatikana ambaye bodi ya wakurugenzi ilipeleka jina lake mamlaka za juu kwa hatua za kuidhinishwa lakini majibu hayajarudi hadi sasa.
“Hata juzi kwenye kikao cha bodi tulikuwa tunalizungumzia hilo kwa kuhoji hii ‘veting’ mbona imechukuwa muda mrefu sana. Kwa hiyo kwa sasa hivi bado hatujapata majibu hata huyu anayekaimu amechoka kutokana na majukumu kumwelemea hivyo ametuomba tufanye utaratibu mwingine wa kumkaimisha nafasi hii mtu mwingine.
“Kwa hiyo jina hadi sasa lipo serikalini kwa maana ya uchunguzi zaidi ili kuhakikisha mtu huyo ni safi na anafaa kuongoza nafasi hiyo.
“Tumeshaulizia wizarani nao wakatujibu wamepeleka jina utumishi ambao nao wamejibu bado wanafanyia uchunguzi kwa hiyo tunasubiri majibu baada ya kumalizika kwa ‘veting’,” alisema Sabuni.
Alipoulizwa kuhusu Mwanasheria Mkuu VETA kukaimishwa ukurugenzi wa kitengo ambacho hana utaalamu nacho alisema huo ni uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Profesa Idris Mshoro, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema huo ndio uamuzi uliofikiwa.