Na MWANDIHI WETU, DODOMA
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyoagizwa na Serikali.
Magereza Mkoa wa Dodoma ilipewa Sh milioni 24 na Serikali kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu Sh 50,000.
Uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambako dawati moja limegharimu Sh 70,000.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana alipotembelea Gereza la Isanga mjini Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.
Alisema kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo isingepelekwa kwenye taasisi nyingine ya umma.
Kwa sababu hiyo alimtaka Rugimbana kufuatilia ziada ya Sh 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati ilitoka wapi na ilikwenda kwa nani.
“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali.
“Serikali imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwamo za jeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwamo madawati ili kuziongezea tija,” alisisitiza.