KINSHASA, DRC
TUME ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetangaza kuwa uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Novemba mwaka huu, sasa utafanyika miaka miwili ijayo.
Viongozi kadhaa wa upinzani walioshiriki katika mazungumzo ya amani wameafikiana na uamuzi huo, lakini wengine wanasema ni njama ya Rais Joseph Kabila kubakia madarakani.
Lakini Tume ya Uchaguzi imesisitiza kwamba haiwezekani kufanya uchaguzi mwaka huu kama ilivyoelezwa kwenye Katiba na badala yake utafanyika Novemba 2018.
Awali mchakato wa kufanyika kwa uchaguzi ulitarajiwa kuanza jana kabla ya kusogezwa.
Lakini pia makundi ya upinzani yamepanga maandamano kupinga kuandaliwa kwa kalenda mpya ya uchaguzi.
Maandamano kama hayo kipindi cha wiki kadhaa zilizopita yameshaua watu zaidi ya 100 na kujeruhi wengine wengi.
Tayari Marekani imewataka maofisa na raia wake kuondoka nchini hapa kwa hofu ya kutokea machafuko makubwa.
Kabila amekuwa madarakani kwa mihula miwili tangu mwaka 2001, lakini inamzuia kuwania muhula wa tatu na hajatangaza hadharani mustakabali wa maisha yake ya kisiasa.