RAIS wa Philippines, Rodrigo Duterte, amejifananisha na Kiongozi wa zamani wa Ujerumani, dikteta Adolf Hitler, aliyewaua Wayahudi milioni sita, kwa kuahidi kuwaua watumiaji wa dawa za kulevya milioni tatu waliopo hapa.
Duterte alisema atafurahi akiangamiza mamilioni ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini hapa, hatua ambazo alishaanza tangu aapishwe kuwa rais Juni 30, mwaka huu.
Tayari ameshawaua watuhumiwa 3000 wa mihadarati na wengine karibu 700,000 wamejisalimisha wenyewe na ameomba muda wa miezi sita zaidi ili kumaliza kazi yake hiyo.
Wafuasi wake na raia wa Philippines waliokuwa wamechoshwa na kuenea kwa uhalifu, wamepongeza hatua zake ngumu.
Hata hivyo, amezidi kupata ukosoaji kutoka kwa jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani, wakisema ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Duterte amewaeleza wakosoaji wake hususan Umoja wa Ulaya kuwa ni ‘kundi la wapuuzi’ na kwamba Marekani ambayo ni mshirika wake wa siku nyingi na mataifa ya Ulaya yanachofanya ni unafiki tu.
Kauli yake ya sasa ambayo ni kali zaidi tangu aanzishe vita yake dhidi ya uhalifu, aliitoa mapema juzi alipowasili katika mji wake wa nyumbani wa Davao, akitokea ziarani nchini Vietnam alikofanya majadiliano juu ya kampeni yake na namna Serikali zinavyoweza kupambana na uhalifu wa kimataifa ikiwemo dawa za kulevya.
Duterte aliwaambia waandishi wa habari kuwa wakosoaji wake wamekuwa wakimchukulia kama binamu wa Hitler.
“Kuna mateja milioni tatu Philippines. Nitafurahia kuwachinja wote. Kama Ujerumani ilikuwa na Hitler aliyeua Wayahudi wasio na hatia, Philippines itakuwa na mimi nikichinja wahalifu,” alinukuliwa akisema.