Na JUDITH NYANGE,
MAITI mbili kati ya 13 zilizopatikana kutokana na ajali ya Hiace na basi la Super Shem wilayani Kwimba zimehifadhiwa chini katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa vile hospitali hiyo haina chumba cha kuhifadhia maiti.
Miili hospitalini hapo huhifadhiwa katika chumba kidogo cha muda chenye uwezo wa kuhifadhi miili minne tu kwa kulaza sakafuni.
MTANZANIA ilishuhudia maiti tatu zikiwamo mbili za ajali ya iliyohusisha basi la Super Shem lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Mwanza na Hiace iliyokuwa ikitoka Kata ya Shirima wilayani Kwimba, ikiwa imelazwa sakafuni ndani ya chumba kidogo kinachotumia kuhifadhia maiti Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Mwamaya.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Misungwi, Florah Kuzenza, alisema wanalazimika kutumia chumba kidogo kuhifadhi maiti kwa dharura kwa sababu hospitali hiyo haina chumba wala vifaa vya kuhifadhi maiti.
“Maiti zinapopatikana tunalazimika kuzichoma sindano ili zisiharibike na kuzihifadhi sakafuni katika chumba tunachokitumia kama mortuary hata maiti tulizozipokea mapema leo (juzi) asubuhi tumezihifadhi katika chumba hicho.
“Zinapopatikana maiti zaidi ya nne au inapotokea ajali kubwa na kuua watu wengi na maiti zikaletwa hapa, tunalazimika kuhamisha vitu vilivyopo katika chumba cha wodi ya wanaume pamoja na wagonjwa na kuitumia wodi hiyo kuhifadhi maiti hizo kwa kuzipanga sakafuni,” alisema Kuzenza.
Kuzenza alisema maiti inapopatikana wanajitahidi kutafuta ndugu wa marehemu waweze kuchukua miili za ndugu zao na zinazopatikana za kuokotwa barabarani na kuletwa hospitali zikaa zaidi ya siku mbili bila kutambuliwa hulazimika kuomba kibali polisi na kuzika katika eneo la hospitali.
Alisema kwa Septemba pekee wameshazika zaidi ya maiti tatu katika eneo la hospitali baada ya kushindwa kutambuliwa na kukosa ndugu.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, alisema ofisi yake inalifahamu suala hilo na tayari wamepatikana wafadhili na hivi sasa unatafutwa ushauri na kuangalia vyumba vya kuhifadhia maiti vilivyopo katika hospitali nyinginea ili kuanza ujenzi Januari, 2017.
“Tunatafuta ushauri kutoka Hospitali ya Temeke, Amana na Muhimbili ili jengo tutakalojenga liwe la kisasa na liendane na wakati tuliopo,” alisema Sweda.