ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, anaelekea kupata hifadhi nchini Afrika Kusini baada ya taifa hilo kukubali kumpokea.
Machar yuko mjini Khartoum baada ya kuondolewa kutoka umakamu wa rais ghasia zilizozuka mjini Juba kati ya vikosi vyake na vile vinavyomtii Rais Salva Kiir.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ya Kenya, Manoah Esipisu, Kenya ilishiriki katika mazungumzo ya ni wapi Machar anapaswa kupatiwa hifadhi na kubaini kuwa Afrika Kusini iko tayari kumpokea.
Pia amesema makubaliano yalifikiwa wiki iliyopita kwa Kenya kutuma wanajeshi zaidi nchini Somalia kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kati ya Septemba 24 na Oktoba 10 nchini humo.
Esipisu alikuwa akijibu maswali kwa wanahabari kuhusu hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuahirisha mipango yake ya kusafiri kwenda New York kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa (UN).
Alisema uwepo wa Kenyatta ni muhimu katika kukabiliana na hali ya Somalia na ile ya Sudan Kusini.
Naibu wa Rais William Ruto anamwakilisha Rais Kenyatta katika mkutano huo wa UN.