Na MWANDISHI WETU,PEMBA
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iko mbioni kuanzisha mfuko wa hija kuwawezesha Waislamu wasiokuwa na uwezo lakini wana nia ya kwenda kutekeleza ibada ya hija.
Katika hotuba yake ya Baraza la Iddi jana, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapindunzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema mfuko huo pia utasaidia wastaafu ambao wamekuwa wakitumia fedha zao za kiinua mgongo kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada ya hija Makka, Saudia Arabia.
Dk. Shein aliyaeleza hayo katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkanyageni Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba alipozungumza na waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria baraza la Iddi ambalo kitaifa limefanyika kisiwani humo.
Ili kufanikisha suala hilo, Dk. Shein alizitaka taasisi zinazojihusisha na kupeleka mahujaji kushirikiana na Serekali kupitia Kitengo cha Wakfu na mali amana kuhakikisha waislamu wanaokwenda kufanya ibada ya hijja wanakwenda na kurudi salama.
Alisema Sh bilioni 16 .2 zimelipwa kwa wastaafu 1,193 na kati yao, 90 wamepewa fursa maalum kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada ya hija ambayo ni nguzo mojawapo katika nguzo za kiislamu.
“Ni vema taasisi zinazochughulika na usafirishaji wa mahujaji kuendelea kushirikiana na serikali kupitia kitengo cha wakfu na amali amana kuhakikisha mahujaji wanapata huduma muhimu wakati wote wanapotekeleza ibada hiyo,” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein pia aliwaasa Waislamu kuendelea kudumisha amani ya nchi kwa kutii sheria ambayo ndiyo msingi katika kuleta mshikamano wa wananchi hivyo kufikia maendeleo.