SERIKALI imetakiwa kuwekeza katika ngoma za asili ili wasanii wa muziki wa Bongo Fleva waache tabia ya kukana nyimbo zao za asili na kuiga muziki wa nchi nyingine ambao hutokana na nyimbo za asili za nchi zao.
Kuiga huko kumeelezwa kunasababisha kupoteza ladha na uhalisia wa muziki wa Tanzania.
Wito huo umetolewa wakati wa tamasha la muziki wa Asili Isimila lenye lengo la kutangaza na kudumisha muziki wa asili lililofanyika wiki iliyopita mkoani Iringa ambapo liliwakutanisha zaidi ya wasanii 100 kutoka ndani na nje ya mkoa huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa Tamasha hilo, Josephine Smith, alisema lengo la kuanzisha tamasha hilo ambalo ni la kwanza kufanyika Nyanda za Juu Kusini, ni kuongeza heshima kwa muziki wa asili kwa kuwa kuna hatari kubwa ya kuupoteza kutokana na kukua kwa utandawazi.