NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka Benki ya CRDB kuendelea kubuni huduma ambazo zitawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi hasa waishio vijijini.
Alikuwa akizungumza   wakati wa uzinduzi wa kituo cha kisasa cha kutolea huduma cha benki hiyo.
Alisema sera ya serikali ni kujumuisha wananchi wengi zaidi katika mfumo halali wa fedha.
Mbali ya kituo hicho, benki hiyo pia ilizindua kadi ya kimataifa ya ‘Tembocard Visa Infinite’ ambayo itamwezesha mteja kupata huduma mbalimbali za kimataifa popote  duniani.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha makundi yote ya  jamii hasa ya vijijini yanafikiwa na huduma za fedha ili kuwakomboa na umaskini, hivyo endeleeni kuwa wabunifu,” alisema Dk. Ackson.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk. Charles Kimei, alisema kituo hicho cha kisasa kimeanzishwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya huduma za fedha kwa wateja wakubwa na wa kati na kwamba hadi sasa kina wateja 8,000.
“Kituo kimejengwa katika viwango vya kimataifa  kuendana na hadhi ya wateja tuliowalenga, mteja atahudumiwa na mhudumu maalumu na kwa muda mfupi,” alisema Dk. Kimei.
Alisema huduma nyingine   katika kituo hicho ni kuwekeza ndani na nje ya nchi, riba nafuu kwa huduma za uwekezaji, kipaumbele kwenye mikopo na kuunganishwa na njia mbadala za utoaji huduma.
Awali, Mkurugenzi wa Masoko wa benki hiyo, Tully Mwambapa, alisema kadi ya kimataifa ya ‘Tembocard Visa Infinite’ inamwezesha mteja kupata bima ya safari na huduma nyingine na kama ikipotea hutumiwa nyingine pale alipo pamoja na kupatiwa fedha za dharura.