Na PAULINA KEBAKI,DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wadogo wanaouza bidhaa za viwanda vya Kampuni ya TBL Group nchi nzima wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali yaliyoondaliwa na kampuni hiyo kupitia mpango wa kuendeleza wajasiriamali wadogo inaoshirikiana nao ujulikanao kama ‘Retail Development Programme (RDP).
Mkurugenzi wa Mauzo na Usambazaji wa TBL Group, Gareth Jones, alisema Dar es Salaam jana kuwa mafunzo hayo katika awamu ya kwanza yatawafikia zaidi ya wafanyabiashara 1,838 kutoka kanda mbalimbali za mauzo ya kampuni hiyo nchi nzima.
“Mafunzo hayo yataendelea kwa miezi mitatu kuanzia sasa ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa kampuni wa kuwawezesha wabia inaoshirikiana nao biashara kwa kufikisha bidhaa inazozalisha kwa walaji wa mwisho.
“Lengo ni kuwawezesha waendeshe biashara zao kwa weledi na kupata mafanikio katika biashara zao” alisema Jones na kuongeza:
“Mtazamo na moja ya malengo ya kampuni mama ya SABMiller ni kujenga ‘Dunia Yenye Nuru Njema’.
“Hii imelenga kuharakisha ukuaji wa maendeleo ya jamii kwa kuhakikisha wabia wanaouza bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyake hususan wafanyabiashara wadogo wanawezeshwa kustawisha biashara zao ikiwamo kuwawezesha kuishi maisha bora na familia kupitia biashara zao na kutoa mchango wa kuendeleza jamii wanazoishi na kufanyia biashara zao”.
Mafunzo yatakayotolewa kwa wafanyabiashara hao ni kuhusiana na mbinu za kufanikisha mauzo na nidhamu katika matumizi ya fedha, mahesabu sahihi katika biashara.
Mengine ni utunzaji sahihi wa vitabu vya hesabu na mbinu za kukabiliana na ushindani wa biashara ya uuzaji vinywaji na ujasiriamali kwa ujumla.
Katika mafunzo hayo, wafanyabiashara wanafundishwa masuala ya usafi na mazingira katika maeneo yao ya biashara na kanuni nyinginezo ikiwamo taratibu za uendeshaji biashara kwa kushirikiana na kampuni ya TBL Group na kutambua bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo na kampuni zake tanzu.