KURA mpya ya maoni imegundua Wajerumani wamegawanyika iwapo Kansela, Angela Merkel awanie muhula wa nne madarakani ambapo wengi wanamshutumu kwa sera yake ya kukaribisha wakimbizi nchini hapa.
Kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni iliyochapishwa juzi na gazeti maarufu la Ujerumani la Bild am Sonntag, umashuhuri wa Merkel umeshuka baada ya asilimia 50 kupinga kutumikia muhula wa nne madarakani baada ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Mlolongo wa mashambulizi dhidi ya raia Julai mwaka huu, ambapo mawili kati yao yalidaiwa kuwa na mkono wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) yamemuweka katika wakati mgumu kiongozi huyo.
Inatokana na sera zake kuwafungulia milango wahamiaji, ambao imewaruhusu mamia kwa maelfu kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na kwingineko kuingia Ujerumani mwaka jana.
Nusu ya watu 501 waliohojiwa na kampuni ya Emnid iliofanya uchunguzi huo wa maoni kwa niaba ya gazeti hilo wasingependa kuona Merkel anaendelea kubakia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 wakati asilimia 42 wakitaka aendelee kubakia.