Na MWANDISHI WETU, MPANDA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema wakimbizi waliopewa uraia wa Tanzania na kuutumia vibaya, watanyang’anywa uraia huo na kurudishwa walikotoka.
Kutokana na hali hiyo, amewataka raia hao wa Tanzania kuendelea kukumbushana juu ya umuhimu wa amani ili waendelee kuishi kama Watanzania wengine.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waliokuwa wakimbizi wa Burundi ambao kwa sasa wamepewa uraia wa Tanzania wanaoishi katika Kata ya Katumba, Halmashauri ya Nsimbo, wilayani Mpanda, mkoani Katavi.
“Wakimbizi waliopewa uraia wameendelea kuingiza ndugu zao. Naagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ifanye ukaguzi katika kambi zote kwa sababu zimegeuzwa kuwa maficho ya kuwahifadhi watu wanaoingia nchini bila ya vibali.
“Hakikisheni mnachukua hatua kwa wote watakaoingiza watu kinyemela katika Kambi za Wakimbizi za Mishamo na Katumba. Pia msiruhusu watu kuleta silaha kwenye maeneo haya kwa sababu Tanzania watu wanaoruhusiwa kutembea na silaha ni askari tu,” alisisitiza Waziri Mkuu.